Buha FM Radio
Buha FM Radio
December 3, 2025, 5:07 pm

Madiwani wa Kata mbalimbali katika Halmashauri ya Mji Kasulu wameahidi kusimamia miradi yote ya maendeleo pamoja na kusimamia ukasanyaji wa mapato katika Halmashauri hiyo ili kuiwezesha serikali kujitegemea kupitia mapato ya ndani.
Na; Sharifat Shinji
Madiwani wateule katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma amekula kiapo cha kuwatumikia wananchi wa halmashauri hiyo huku wakiahidi kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato katika kata zao.
Zoezi hilo la uapisho limefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mbele ya Hakimu mkaazi mwandamizi wa mahakama ya Wilaya, Iman David Matenzi, ambapo baadhi ya Madiwani hao akiwemo Elisha Bakena Diwani wa kata ya Mrusi, ameahidi kusimamia miradi ya maendeleo kwa uadilifu, kuwasimamia wananchi kikamilifu pamoja na kutatua migogoro ya wananchi katika Kata zao.
Awali akitoa salamu kutoka mkoani Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Ndg. Elisante Mbwilo amewataka Madiwani kwenda kuwatumikia wananchi bila upendeleo pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato kama ilivyoagizwa na Rais kuwezesha serikali kujitegemea kiuchumi na kuwezesha Halmashauri kuongeza mapato na kumudu gharama uendeshaji wa Miradi yake.

Aidha amewataka madiwani hao kushirikiana kwa miaka yote mitano ili kuleta usawa, uwazi, uadilifu na utawala wa sheria ili kuleta matumizi bora ya rasilimali katika Halmashauri hiyo kwa misingi ya maendeleo endelefu.
Katika hatua nyingine Evelin John ambaye ni Diwani wa viti malumu kutoka kata ya Heru Juu amesema ataenda kusukuma usimamizi wa masoko yote ya kimkakati wanayasimamia kimamilifu ili kuleta mapato katika Halmashauri pamoja na kuanzisha vikundi vya watu wa jinsia zote ili wananchi wanufaike na miradi mikopo ya Halmashauri.

Hata hivyo madiwani hao wamemchagua kwa kumpigia kura Ayubu Ngalaba kuwa mwenyekiti wa barazahilo linaloundwa na Madiwani wa kata 15 pamoja na madiwani wa viti maalumu kukamilisha madiwani 20 huku Ndg. Ayubu Mgalaba akiahidi kusimamia kwa uadilifu Baraza hilo.
