Buha FM Radio
Buha FM Radio
August 22, 2025, 7:32 pm

Miundombinu katika kata ya Buhoro Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetajwa kuwa ni sababu inayopelekea vijana wengi kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya uzalishaji mali jambo linalosababisha kukosa maendeleo katika eneo hilo.
Na; Paulina Majaliwa
Baadhi ya vijana katika kata ya Buhoro Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wemeeleza sababu mablimbali zinazokwamisha shughuli zao za uzalishaji mali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi ndani ya jamii.
Wamesema hayo wakati wakizungumza na Buha Fm redio leo ambapo wamesema ubovu wa miundombinu kama vile shule, barabara, zahanati, uhaba wa masoko pamoja na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali ni miongoni mwa vikwazo kwa vijana wengi kujikwamua kiuchumi.
Aidha wameongeza kwa kusema ukosefu wa huduma mhimu katika baadhi ya maeneo katika vijiji vinavyounda kata hiyo hupelekea vijana kujiingiza katika shughuli haramu ikiwemo wizi, upolaji mali pamoja na makundi yasiyofaa katika jamii.
“kuna vitu vingi vya kuboresha katika kata yetu ya Buhoro kwa sababu tunaona kama sisi tumetelekezwa hasa kwenye miundombinu mhimu jambo linalopelekea vijana wengi kukosa kazi malumu na kujikuta wanaingia katika shughuli haramu kama vile wizi upolaji, na vitendo vya ubakaji kutokana na kukosa shughuli za kufanya katika kata yetu” Wamesema Vijana hao.

Kwa upande wake katibu wa vijana Staford Michael amesema kuwa ushirikishwaji wa vijana katika kuleta maendeleo ndani ya jamii ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili katika idara hiyo kutokana na mwitikio wa vijana katika shughuli za kijamii.
“vijana hatushirikishwi kwa baadhi ya mambo yanayotendeka kwenye jamii zetu kutokana na mwitikio wetu kuwa ndogo mfano kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hizo nafasi hatupati pia tunaachwa nyuma kwa mambo mengi sana hivyo vijana tukianza kujitokeza kwa wingi pengine ilkaleta tija katika kata yetu” Amesema Staford.
Pia amesema baadhi ya viongozi wanashindwa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa hivyo amesema serikali ichunguze baadhi ya viongozi kulingana na nafasi zao pia utendaji wao wa kazi.
katika hatua nyingine baadhi ya wananchi katika kata hiyo akiwemo Adriano Msase na Saraphina Mlanga wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara, maji, shule pamoja na miundombinu ya afya pia wamewaasa vijana hao kufanya kazi kwa kujituma ili kufikia malengo na kutimiza ndoto zao.

Buhoro ni miongoni mwa Kata 21 zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya kasulu katika Mkoa wa Kigoma ambapo katika sensa iliyofanyika mwaka 2012, kata hiyo ilikuwa na wakazi wapatao 60,120 na katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata hiyo walihesabiwa kuwa 17,072.