Buha FM Radio
Buha FM Radio
June 14, 2025, 4:22 pm

Afisa ardhi wa halmashauri ya mji Kasulu Pesha Jackson ameeleza bado kuna mwitikio mdogo kwa wananchi ndani ya halmashauri ya mji Kasulu katika swala la ukataji wa hatimiliki ukilinganisha na viwanja vyenye sifa ya kukatiwa hati na kuwaomba wananchi kuendelea kujitokeza katika ofisi za ardhi na kukata hatimiliki za maeneo yao.
Wananchi wa halmashauri ya mji Kasulu mkoani Kigoma wameshauriwa kukatia hatimiliki ardhi zao ili kupunguza migogoro ya ardhi miongoni wa wakazi na kutambulika kisheria. wito huo umetolewa na Afisa ardhi wa halmashauri ya mji Kasulu Pesha Jackson wakati akiongea na Buha FM Radio juu ya umuhimu wa kuwa na hatimiliki ambapo amefafanua kuwa hatimiliki inamsaidia mwananchi kuwa na utambulisho wa eneo lake la ardhi kisheria na kumpa fursa ya kuitumia katika udhamini wowote ikiwa ni pamoja na kukopesha fedha kutoka sehemu yoyote.
Aidha, ameeleza kuwa bado kuna mwitikio mdogo kwa wananchi ndani ya halmashauri ya mji Kasulu katika swala la ukataji wa hatimiliki ukilinganisha na viwanja vyenye sifa ya kukatiwa hati na kuwaomba wananchi kuendelea kujitokeza katika ofisi za ardhi na kukata hatimiliki za maeneo yao.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa halmashauri ya mji Kasulu wameiomba serikali kupitia ofisi ya ardhi kuendelea kutoa elimu juu ya maswala ya umiliki wa ardhi kwani wengi wao hawana uelewa mpana kuhusu jambo hilo hali inayosababisha kushindwa kwenda kukata hatimiliki kwa ajili ya maeneo yao .