Taasisi zisizo za kiserikali Kusini Unguja zachochea maendeleo Kizimkazi
12 August 2023, 1:43 pm
Wakazi wa kijiji cha Kizimkazi Mkunguni wilaya ya Kusini Unguja wameendelea kunufaika na mafunzo na miradi inayotolewa na taasisi zisizo za kiserikali kijijini kwao.
Na Miraji Manzi Kae
Kuwepo kwa taasisi zisizo za kiserikali zinazofuata taratibu za maeneo husika kuwawezesha kuleta maendeleo makubwa katika jamii na kufaidika kielimu na kiuchumi.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja mhe. Rashid Hadid Rashid alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Asalaam Community iliyopo kijiji cha Kizimkazi Mkunguni inayojishughulisha na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo elimu na ujasiriamali.
Mhe. Rashid amesema kuwa serikali inathamini michango inayotolewa na jumuiya hiyo kwani imeonesha nia ya kusaidia walio wengi bila kujali jinsia, rangi wala dini.
Jumuiya hiyo inayoongozwa na Bi. Khadija Colak kutoka Uturuki inasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na elimu kwa watoto yatima jambo ambalo linaleta faraja kwa wakazi wa Kizimkazi na vijiji jirani.
Mhe. Rashid alikutana na kamati ya sherehe Kizimkazi day ili kujua maandalizi ya sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni kijijini hapo.