Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
September 3, 2025, 6:40 pm

Kufuatia hadha ya muda mrefu kwa baadhi ya wakazi wa wilaya za Kyerwa,Karagwe na Missenyi mkoani Kagera kuvamiwa na tembo, kuharibu mali, mazao na kusababisha vifo vya watu, mamlaka ya uhifadhi nchini (TANAPA) imeanza zoezi la kuwaondoa Tembo hao na kuwarudisha katika maeneo yao ya asili kwenye hifadhi ya taifa ya Brigi-Chato.
Na Anold Deogratias
Serikali kupitia mamlaka ya uhifadhi nchini (TANAPA) imeanza zoezi la kuwaondoa Tembo zaidi ya 500 katika ranchi ya kitengule na karibu na makazi ya watu katika wilaya za Karagwe, Missenyi na Kyerwa na kuwarudisha katika maeneo yao ya asili kwenye hifadhi ya taifa ya Brigi-Chato.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika katika mashamba ya miwa ya Kagera, mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amewahakikishia wananchi kuwa tatizo la uvamizi wa Tembo katika makazi yao linakwenda kuisha hivyo amewataka askari wa uhifadhi kufanya kazi hizo kwa uweledi ili zoezi lifanikiwe.
Sauti ya mkuu wa mkoa wa Kagera Fatm Mwassa

Awali akitoa taarifa mhifadhi mkuu, hifadhi ya Ibanda-Kyerwa, Dkt.Frederick Mofulu amesema kuwa Tembo hao wameloea katika ranchi ya kitengule na maeneo mengine kwa zaidi ya miaka 18, na kwamba eneo hilo ni dogo na hakuna malisho ya kutosha hivyo kulazimika kuvamia makazi ya watu na mashamba ya miwa ya kiwanda cha Kagera.
Sauti ya mhifadhi mkuu, hifadhi ya Ibanda-Kyerwa, Dkt.Frederick Mofulu

Naye meneja wa kilimo wa kiwanda cha Kagera eneo la kitengule Bw.Lebahati Emmanuel amesema kuwa kwa mwaka jana na mwaka huu Tembo hao wameharibu hekta 773 na kusababisha hasara ya tani laki 2 za sukari sawa na hasara ya shilingi bilioni 6.
Sauti ya meneja wa kilimo wa kiwanda cha Kagera eneo la kitengule Bw.Lebahati Emmanuel
Akiongea kwa niaba ya wenyeviti wa vijiji vinavyoathiriwa na Tembo hao, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakashenyi kata ya Businde wilaya ya Kyerwa Bw.Jackson Cosmas Mkundane amesema kuwa wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao ya wananchi, pamoja kuua baadhi ya wananchi.
Sauti ya mwenyekiti wa kijiji cha Nyakashenyi Bw.Jackson Mkundane
Zoezi hilo litafanyika katika wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi mkoani Kagera.
