Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
August 12, 2025, 11:05 pm

Watanzania wametakiwa kuwasikiliza kwa umakini na kupima uwezo wa wagombea pindi watakapoenda kuomba kura kwa wananchi ili kuhakikisha wanamchagua mtu sahihi wa kuwaletea maendeleo.
Na Anold Deogratias
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Dotto Biteko amewataka Watanzania kuwapima wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao kama wanafaa kuwaletea maendeleo na kuchagua kwa haki ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.
Dk Biteko amesema hayo, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera yaliyofanyika katika Viwanja vya Kanisa Kuu Yohana Mbatizaji – Murgwanza, wilayani Ngara mkoani Kagera.

Amewataka watanzania kuwasikiliza kwa umakini wagombea watakapokuwa wanajinadi na baada ya hapo watambue ni yupi atawaletea maendeleo lakini pia amesisitiza uchaguzi uziwagawe kwani suala la uchaguzi ni la muda.
Sauti ya Naibu Waziri Mkuu na waziri wa nishati Dkt.Dotto Biteke
Awali akiongea wakati wa sherehe hiyo Askofu wa Dayosisi hiyo Darlington Bendankeha ameomba ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kipande cha mita 900 zinazoingia katika hospitali ya Murgwanza, pamoja na gari la kubebea wagonjwa hospitalini hapo.
Sauti ya Askofu Darlington Bendankeha

Akijibu maombi hayo Dkt.Biteko ameuagiza uongozi wa wilaya, mkoa na mamlaka za barabara mkoa wa Kagera kuhakikisha kuwa kipande hicho kinatengenezwa kwa kiwango cha lami na pia ameahidi kuwa serikali kupitia wizara ya Afya watapeleka gari la wagonjwa hospitalini hapo.
Sauti ya Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma A. Mwassa ameushukuru uongozi wa Kanisa hilo kwa ushirikiano mkubwa kati yake na Serikali katika utoaji wa wa huduma kwa wananchi hususani katika Sekta za Afya, Elimu na huduma za Jamii kupitia shule na hospitali zinazotoa huduma kwa wananchi pamoja na huduma za kiroho zinazotolewa na kanisa hilo kwa wananchi wa Kagera.

Katika sherehe hizo za maadhimisho ya miaka 40 ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera ziliambatana na harambee ya ujenzi wa Kanisa kuu la Dayosisi hiyo iliyoongozwa na Mhe. Naibu Waziri Mkuu ambapo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia shilingi milioni 50 na Naibu Waziri Mkuu amechangia mifuko 1000 ya saruji.