Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
July 31, 2025, 6:00 pm

Serikali imeombwa kuufanya Mkoa wa Kagera kuwa Kanda Maalum ili kukabiliana na majanga ambayo yamekuwa yakiukumba mkoa huo mara kwa mara ikiwemo magonjwa na majanga ya asili.
Na Anold Deogratias
Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima ameiomba serikali kuutambua mkoa wa Kagera kama kanda maalum katika kukabiliana na maafa kutokana na majanga yanaoukumba mkoa huo mara kwa mara.
DC,Siima amesema hayo hivi karibuni wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya kamati elekezi na kamati ya wataalam ya maafa katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambapo ameeleza kuwa mkoa wa Kagera umekua ukikumbwa na maafa ya mara kwa mara ikiwemo tetemeko la ardhi,mvua za upepo mkali, radi na magonjwa ya mlipuko kama maburg na kipindupindu.

Kufuatia hali hiyo Mh. Sima ameeleza kuwa ghala la sasa la kukabiliana na maafa lipo mkoani Shinyanga hivyo panapotekea tatizo inachukua muda mrefu kusafirisha vifaa vya uokozi pamoja na mahitaji mbalimbali kwa waathirika, Hivyo kupelekea kuiomba Serikali iangalie namna ya kuufanya mkoa wa Kagera kuwa kanda maalum kwa kuipatia ghala la kupambana na maafa pamoja na wataalam.
Sauti mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Siima
Nae mwezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Winniefrida Ngowi amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kamati za maafa za wilaya zinajiandaa kikamilifu na kuchukua hatua stahiki za kuzuia majanga yanayoepukika na kuaandaa mipango madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili kama tetemeko na mafuriko.
Sauti ya mwezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Winniefrida Ngowi

Nae mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Fatina Hussein Laay, amewashukuru wawezeshaji kutoka ofisi ya waziri mkuu kwa kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania kwa kuendesha mafunzo hayo na kuahidi kamati ya wataalam kutoka ofisi yake itayafanyia kazi yale yote waliyojifunza.

Itakumbukwa mnamo miaka ya 1980 virusi vya UKIMWI viligunduliwa mkoa wa Kagera, tarehe 10,09, 2016 tetemeko la aridhi lilitokea mkoa wa Kagera na kupelekea vifo vya watu 19, mwaka 2023 na mwaka 2025 ugonjwa wa Marburg uligunduliwa katika wilaya za Bukoba na Biharamulo, mlipuko wa kipindupindu mwaka 2024, lakini pia mvua kubwa na upepo mkali vimekuwa vikiukumba mkoa wa Kagera mara kwa mara.