Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
July 26, 2025, 3:55 pm

Waziri wa maji, Jumaa Aweso, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Lwakajunju uliopo wilayani Karagwe, kutatua changamoto zinazowakabili vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo ikiwemo malipo yao pamoja na kuwapa mikataba.
Na Avitus Kyaruzi
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametoa maagizo kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa miji 28, wa Lwakajunju wilayani Karagwe, mkoani Kagera kuhakikisha changamoto zinazowakabili vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo ikiwemo malipo yao kulipwa haraka.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo Waziri Aweso amekemea vikali kitendo cha mkandarasi kushindwa kutekeleza wajibu wa kuheshimu haki za wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kutowapa mikataba ya kazi na stahiki zao kwa wakati na kwamba serikali haitavumilia uzembe wa aina hiyo
Sauti ya waziri wa maji Jumaa Aweso
Aidha waziri huyo amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na matunda ya serikali.
Sauti ya waziri wa maji Jumaa Aweso
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo mhandisi Magreth Nyange, ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 64 utekelezaji wake ulianza mwaka 2023 na unatakiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo hadi sasa umefikia asilimia 64, huku Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julis Laiser akisema kuwa mradi huo unakwenda kuondoa changamoto kubwa ya maji.
Sauti ya msimamizi wa mradi mhandisi Magreth Nyange na mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Laiser
Nao baadhi ya wananchi wa wilaya ya Karagwe wameeleza kufurahishwa na uwepo wa mradi huo, wakisema kuwa utatatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yao.
Sauti za wananchi wa wilaya ya Karagwe
Mradi wa maji wa Rwakajunju wa miji 28 unaenda kuwanufaisha wananchi zaidi ya Laki tatu na elfu Hamsini wa kata kumi na mbili za wilaya ya Karagwe.
