Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
June 14, 2025, 10:17 am

Wakulima wa mpunga skimu ya MWISA wilayani Karagwe mkoani Kagera wamepatiwa elimu juu ya kutumia kanuni bora za kilimo ikiwemo kupima afya ya udongo ili kuweza kunufaika na kilimo chao na kukuza uchumi wao.
Na :Anold Deogratias
Wakulima wilayani Karagwe mkoani Kagera wametakiwa kufuata maelekezo ya Maafisa Kilimo na kufuata kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kupima afya ya udongo ili waweze kunufaika na uzalishaji wao.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mhandisi wa Umwagiliaji wa Wilaya ya Karagwe Ndg. Damas Kalisti katika Sikukuu ya Mkulima kwenye Skimu ya Umwagijiaji (MWISA)Bujuruga Wilayani Karagwe ambapo wakulima wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya mafunzo ya vitendo ya kilimo bora cha Mpunga.
Aidha ndug. Kalisti amewataka wakulima kutengeneza vikundi vyenye tija vitakavyowawezesha kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri na Benki za Kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Kilimo Ndg. Titus Fredinand ambaye pia ni Mpima Afya ya Udongo amesema kuwa ili kupata mazao mengi ni vizuri kupima afya ya udongo na kufuata kanuni za kilimo bora cha Mpunga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Skimu ya Umwagiliaji Mwisa ndg. Crodatus Lazaro amewashukuru Maafisa Kilimo kwa Mafunzo waliyowapatia kuanzia kuandaa shamba mpaka kuvuna na ana amini mafunzo hayo yataongeza thamani ya mazao watakayozalisha hasa Mpunga.