Radio Tadio

UNICEF, TADIO, Wizara ya Afya mguu sawa dhidi ya ebola

June 4, 2026, 16:05 pm

Waandishi wa habari kutoka redio mbalimbali nchini wakiwa kwenye mafunzo ya kupambana na ugonjwa wa ebola jijini Dodoma. Picha na Bakari Khalid

Na Bakari Khalid

Watendaji wa redio za kijamii kutoka maeneo mbalimbali nchini wanashiriki mafunzo yaliyoandaliwa na TADIO kwa ushirikiano na UNICEF pamoja na Wizara ya Afya, yenye lengo la kuimarisha maandalizi na mwitikio dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Mkufunzi  kutoka Wizara ya Afya, Bi. Grace Msemwa, amesema umuhimu wa redio za kijamii katika utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, akieleza kuwa vyombo hivyo vina mchango mkubwa katika kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu masuala ya afya ya umma.

Grace Msemwa akitoa mafunzo ya namna kujikinga na ugonjwa wa ebola kwa waandishi wa habari. Picha na Bakari Khalid

Msemwa ameongeza kuwa  redio za kijamii zina nafasi kubwa katika kufikisha elimu ya afya kwa wananchi na kusaidia juhudi za maandalizi, kinga na mwitikio wakati wa dharura za kiafya.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa TADIO, Bw. John Baptist, aliwahimiza wawakilishi wa redio za kijamii kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa afya na maendeleo ili kuhakikisha jamii zinapata taarifa sahihi, za kuaminika na kwa wakati kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za pamoja za TADIO, UNICEF , Wizara ya Afya na wadau wengine  zinazolenga kuimarisha uwezo wa vyombo vya habari vya kijamii katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na changamoto nyingine za afya ya umma.