Triple A FM

Agenda ya usafi ni ya kudumu jijini Arusha-Meya

11 November 2021, 3:47 pm

Meya wa jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe

Na.Anthony Masai,Arusha.

Baada ya kunyooshewa kidole cha malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kuhusu huduma duni za ukusanyaji na uzoaji taka jijini Arusha,Meya wa jiji Maxmillian Iranqhe amefanya kikao kazi na mawakala wa usafi ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.

Meya Iranqhe pamoja na kuwambusha mawakala hao jukumu walilokabidhiwa na halmashauri ya jiji la Arusha,pia amekumbusha lengo la jiji hilo la kuwa kinara katika nyanja mbalimbali kuanzia kwenye usafi, ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wa Mawakala hao kupitia kwa Mwenyekiti wao Julia Mangi wamemhakikishia Mstahiki Meya kuwa azma ya kuifanya Arusha kuwa kinara katika kampeni ya usafi inawezekana na wapo tayari kufanya kazi mchana na usiku kuhakikisha kuwa Jiji hilo linang’aa na kuongoza katika kampeni ya usafi kitaifa .

Aidha wameiomba halmashauri ya jiji la Arusha,kuwaongezea muda wa kandarasi kutoka mwaka mmoja kwa sasa hadi miaka miwili; ili kutekeleza kikamilifu kampeni ya usafi kwa ufanisi na weledi mkubwa.

Kwa muda mrefu sasa wananchi katika jiji la Arusha,wamekuwa na malalamiko ya taka kurundikana mitaani kutokana na changamoto za wakandarasi wa usafi,jambo ambalo limekuwa likielezwa na Halmashauri kwamba ni uhaba wa vifaa unaowakabili wakandarasi hao.

mwisho.