Storm FM

Watu wenye ulemavu bado wana changamoto.

23 September 2021, 6:19 pm

Na Zubeda Handrish:

Shirika lisilo la kiserikali la Internews Tanzania limetoa mafunzo maalumu ya siku mbili ili kuwajengea uwezo wanahabari wa Tanzania kuandika kwa usahihi habari za watu wenye ulemavu zenye mchango katika maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao yamefanyika kuanzia Septemba 22 hadi 23, 2021 huku yakijumuisha waandishi wa habariĀ  kutoka vyombo vya habari vya redio, televisheni, magazeti na vyombo vya mtandaoni (online media).

Mgeni rasmi ambaye ni mkurugenzi wa huduma kwa watu wenye ulemavu kutoka ofisi ya waziri mkuu, Jacob Mwinula aliyefungua mafunzo hayo amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuwasaidia watu wenye ulemavu na wao kama wawakilishi kutoka ofisi ya waziri mkuu wataendelea kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili kuendelea kuandika habari zenye tija za watu wenye ulemavu.

Nae Bi. Josephini Lyengi kutoka ofisi ya waziri mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu amesema kuwa watu wenye ulemavu nchini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kuendelea kuwekewa mipango na mikakati mahususi ili kuzitatua kwa kuzingatia nyakati husika.

Aidha Mratibu wa program kutoka Internews Tanzania,  Shabani Maganga amesema bado elimu inahitajika kwa jamii, ili kundi la watu wenye ulemavu lipate nyenzo ambazo zitawawezesha kumudu maisha yao na kuacha utegemezi, huku akitoa pongezi kwa wanahabari kwa kuendelea kutoa mchango wao kwa kuandika habari zenye tika katika jamii zinazotatua changamoto za watu wenye ulemavu.