Sibuka FM

Maswa: Elimu ya chanjo ya Uviko-19 bado inahitajika sana kwa jamii

18 May 2023, 7:08 am

Kwenye picha ni mmoja wa wananachi wa wilaya ya Maswa akionesha cheti chake baada ya kupata chanjo ya Covid-19

Na Alex.F.Sayi

Wananchi Wilayani Maswa Mkoani Simiyu, wamewashukuru wadau wa afya  Internews na Tadio katika mapambano ya ugonjwa wa Korona kwa kuwakumbusha na kuona umuhimu wa  kupata chanjo ya Uviko-19  ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Kelvine Stivene,  wakati akitolea tathmini ya chanjo ya Korona baada ya kupita miezi miwili tangu achanje chanjo hiyo, huku akiuhakikishia umma kuwa chanjo hiyo haikuwa na madhara yoyote na haina uhusiano wowote na nambari 666.

“Unajua kama Taifa tulipitia mambo mengi na hatukua na mwelekeo wa kuchanja na hata tulipoamua kuchanja bado kulikuwa na mitazamo mingi kuhusiana na chanjo hiyo wengine walisema chanjo ni ya freemanson, wengine wakasema ni 666”. Alisema Kelvin

Akizungumza na Sibuka Fm  Denis Kitwala (33)   amesema kuwa tangu apate  chanjo hiyo hajaona madhara yoyote ya kiafya yanayosababishwa na chanjo hiyo na kusema kuwa afya yake inaendelea  vizuri tangu alipochanja chanjo hiyo zaidi ya  miezi miwili sasa.

“Watanzania wasisikilize maneno ya mtaani hizi Chanjo ni salama mimi ninazaidi ya miezi miwili  sasa tangu nimechanja lakini sijaona shida yoyote kiafya hizi Chanjo zingekuwa na madhara kiasi hicho kama wanavyosema tungekuwa tumesha kufa Brother”.Alisema Kitwala.

Kwa upande wake Bi Rosemary Tunge, amesema kuwa bado kuna ulazima wa kuchanja chanjo hiyo kwa kuwa hata waliochanja wanaendelea vizuri na maisha yao na  hakuna madhara yaliyojitokeza kwao hadi sasa.

“Kwa sasa sina mashaka tena na chanjo kwa kuwa waliochanja tunawaona wanaendelea na maisha yao kama kawaida unajua awali nilikuwa ninasita kwa kuwa walisema Chanjo hizi zimeletwa kufanyiwa majaribio.” Alisema Bi,Rose.

Aidha akitolea tathmini ya ufanisi wa chanjo ya korona wilayani Maswa Afisa Afya na  Mratibu msaidizi wa Chanjo Wilaya , Salima Mahizi amesema kuwa zoezi la uchanjaji limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya maambukizi wilayani hapo ambapo uwepo wa washirika wa afya Internews na Tadio wameweza kuwafikia wananchi kwa wingi na urahisi katika zoezi la chanjo.

Kiukweli kwa sasa wilaya ipo salama ikilinganishwa na kipindi ambapo tulikuwa hatujawa tayari kutumia chanjo hizi, nakumbuka kwa siku Hospitali yetu ilikuwa inatoa maiti kumi hadi kumi na tano waliopoteza maisha kwa sababu ya Covid-19, wakati ule tuliwapoteza na baadhi ya watumishi wetu lakini kwa sasa tupo salama.” Alisema Mahizi.

“Uwepo wa wadau wa afya kama Internews na Tadio kupitia redio Sibuka Fm tumefanikiwa kuongeza hamasa kwa watu kujitokeza kupata chanjo hii tofauti na hapo mwanzo kabla ya wadau kuja ,hivyo niwaombe wadau hawa waendelee kuwekeza nguvu kwenye eneo hili’’ Alisema Mahizi