Sibuka FM

Kati ya vifo (100) wilayani Maswa vifo (7)  kati ya hivyo vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

24 March 2023, 8:04 am

Kwenye picha ni afisa lishe wilaya ya Maswa,Abeli Gyunda akiwa studio za redio Sibuka fm wakati wa kipindi cha afya lishe kinachofanyika kila siku ya jumatano

Na Alex .F.Sayi

Imeelezwa kuwa kati ya vifo miamoja Wilayani Maswa Mkoani Simiyu ,vifo Saba kati ya hivyo vinatokana na Magonjwa  yasiyokuwa ya kuambukiza ikiwa ni sawa na asilimia (6.7%) ya vifo vyote Wilayani hapa.

Hayo yamesemwa na Afisa Lishe Wilayani Maswa ,Abel Gyunda ,wakati akizungumza na Sibuka fm  juu ya hali ya ongezeko la wagonjwa wenye Magojwa yasiyo yakuambukiza ikiwemo,Presha(BP),Kisukari,Vidonda vya Tumbo,Saratani, Figo na Ini.

Gyunda amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana (2022) jumla ya wagonjwa (2,372)wagonjwa wa nje waliokuwa wanaendelea kuchukua dawa,kati ya hao wagonjwa wa Presha(BP) walikuwa Wanaume (863)na Wanawake(1,509)na Wagonjwa wa Kisukari walikuwa (671)kati ya hao Wanaume walikuwa (301)na Wanawake wakiwa (370)kati ya wagonjwa (2,372)waliorekodiwa,huku waliolazwa Hospitalini hapo kwa mwaka huo kwa ugonjwa wa Presha(Bp)walikuwa (219)Wanaume wakiwa ni (63)na Wanawake wakiwa ni (116)Ugonjwa wa Kisukari walilazwa wagonjwa (26)Wanaume wakiwa (9)na Wanawake wakiwa (17) huku kukiwa na idadi kubwa ya wanawake wenye magonjwa hayo.

“Ukiangalia takwimu  hizi wanawake wamekuwa wahanga wa maradhi haya,na hii inatokana na mtindo wa maisha kwa sasa inayopelekea kutumia vyakula vingi vya mafuta,matumizi ya Pombe kupita kiasi,matumizi ya tumbaku(Sigara),kutofanya mazoezi nakutokula mlo kamili unaozingatia makundi matano ya lishe,ikiwemo Matunda na Mbogamboga.”Amesema Gyunda.

“ Matumizi ya Pombe yanapaswa kupunguzwa ama kuachwa kwa kuwa kila milligramme (100)ya Pombe ni sawa na asilimia (7%) ya nishati lishe mwilini,ikilinganishwa na Mafuta yenye nishati lishe yenye asilimia (9%)hivyo kufanya ongezeko la uzito wa Mwili  na mafuta mwilini ikiwa kutakuwa na matumizi makubwa ya Pombe na Mafuta’’ Amesema Gyunda

Akizungumzia suala hilo kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa Dkt,Evelini Kisobe amesema kuwa sababu inayopelekea wanawake kuwa wahanga wa maradhi hayo inatokana na tabia ya wanawake wengi kupendelea maisha ya anasa, kula vyakula vya mafuta hasa chipsi,unywaji wa Pombe na Matumizi ya Sigara.

“Ukiangalia mtindo wa maisha kwa sasa unachangia wanawake kupatwa na changamoto hii,kwa kuwa wanawake kwa sasa wanapenda anasa ambazo zamami zilikuwa za wanaume kuvuta Sigara na Ulevi wa Pombe,wanawake pia hawafanyi mazoezi ya mwili kama ilivyo kwa wanaume, wanawake wengi tunabweteka ukiangalia tumezoea kukaa tu Majumbani na hata tulio maofisini tunafanya kazi nyepesi ambazo haziushugulishi mwili tofauti na wanaume ni wachakalikaji.”amesema Dkt,Kisobe.

Naye Bw,Vicent Mapalala msimamizi wa Kituo  cha Afya cha binafsi (Barikiwa)kilichopo Wilayani hapa amesema kuwa wamekuwa wakipokea wagonjwa wenye maradhi yasiyo ya kuambukiza kituoni hapa mengi wao wakiwa ni wanawake.

“Tumekuwa tukipokea wagonjwa wenye shida hiyo na unajua ukiangalia sababu kubwa ya maradhi haya yanatokana na watu kuacha kula vyakula vya asili na sababu nyingine hasa kwa kina mama inatokana na msongo wa mawazo  ukiachilia mbali migogoro ya ndoa wanawake kutelekezewa majukumu yakifamilia lakini pia wanawake ndo wanaoongoza kucheza vikoba mwanamke anaweza akawa na vikundi zaidi ya vitano na vyote hivyo vinataka marejesho kwa wakati hii imechangia mawazo nakupelekea maradhi ya vidonda vya tumbo na Presha (BP)”Amesema Mapalala.

Wakizungumza na Sibuka fm, baadhi ya Wananchi wamekuwa na mitazamo tofauti kama anavyoelezea Bi,Berenadeta Masunga mkazi wa Mtaa wa Majebele miaka (42)amesema kuwa nilianza kuugua Presha nikiwa na Umri wa miaka (27)wakati nilipobeba ujauzito nikiwa Nyumbani hali iliyopelekea kufukuzwa Nyumbani na  kaka zangu wakidai nimewadharau.

“Kiukweli mimi nilifukuzwa Nyumbani na Kaka zangu baada ya kubeba mimba kwa hiyo ikapelekea kuishi maisha magumu sana na nikawa mtu wa mawazo mno siku ya kujifungua nilishindwa kusukuma kama mara tatu nashindwa nilikuwa naishiwa nguvu lakini Mungu alisaidia nikajifungua toka wakati huo ninapresha.”Amesema Masunga.

 “Mimi nakumbuka nilikuwa natumia Majira na nilikuwa natumia Sindano ilikuwa inanisababishia kuishiwa nguvu hadi Nesi mmoja aliponishauri kuacha kutumia  ya sindano, nilipoacha hali ikawa vizuri,huenda kuna baadhi ya kinamama wanaotumia njia za uzazi wa Mpango zinawasababishia Maradhi haya,ukiachilia mbali haya majira kinamama tunatumia vibaya mafuta majumbani na kwenye masherehe maana tunatumia viungo vingi mno na mafuta mengi mno tofauti na wazazi wetu waliokuwa wakitumia mafuta ya Samli na Karanga.”Amesema Masunga.