Sibuka FM

Simiyu: DC Maswa apiga marufuku wanafunzi kufukuzwa shuleni

4 March 2023, 10:18 am

Kwenye picha ni mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Mhe.Aswege Kaminyoge akizungumza na wananchi wa kata ya Nyalikungu wakati wa kikao cha kujadili maendeleo ya kata kilichofanyika katika shule ya msingi Mwawayi

Na Alex Sayi

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu ,Mhe.Aswege Kaminyoge ,amepiga marufuku tabia ya Wakuu wa shule wilayani hapo kuwafukuza wanafunzi kwa sababu  ya kutokukamilisha michango ya shule au kwa sababu zingine zile.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyalikungu wakati wa kikao  cha maendeleo ya Shule kilichofanyika maeneo ya Shule ya Msingi Mwawayi Wilayani hapa.

“Nilishasema ni marufuku walimu wakuu na wakuu shule kuwafukuza wanafunzi shuleni iwe kwa sababu yoyote ile unapomfukuza mwanafunzi unamtengenezea mazingira ya kutokufanya vizuri darasani  na mpaka kupelekea kufeli mitahani yake’’ alisema Aswege Kaminyoge

“Kama kuna kitu ambacho kinamuhusu mwanafunzi naombeni sana aitwe mzazi wa mwanafunzi aambiwe mahitaji au michango ya mwanae na kama akikaidi naomba muniandikie majina ya wazazi ambao wamegoma kuchangia mahitaji ya watoto wao hasa ya shuleni’’alisema Aswege Kaminyoge

Aswege Kaminyoge, amewataka Wenyeviti wa vitongoji kuwa wawazi na kuwashirikisha wananchi kwenye vikao vya maendeleo vinavyofanyika kwa kila mwezi ili wananchi waweze kuchangia shughuli za maendeleo  kwa hiari.

“Wasomeeni wananchi wenu mapato ya michango ya maendeleo ambayo wanachangia katika shughuli za kimaendeleo ili waweze kuona michago yao waliyoitoa kumbe inafanya kazi na hii itawapelekea waweze kuchangia maendeleo kwa hiari ’’ alisema Aswege Kaminyoge

Aidha amewataka watumishi kuchangia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao wanayoishi, hilo limejiri kufuatia hoja iliyoibuliwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Majebele kumweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma kutokuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao wanapoishi.

“Mtumishi wa umma ni lazima uweze kuchangia shughuli za maendeleo katika eneo unaloishi mbona mimi mkuu wa wilaya ninachangia shughuli za maendeleo au mimi siyo mtumishi wa umma ,hata kama hukai eneo hilo lakini taasisi yako ipo eneo hilo ni lazima uchangie ’’ alisema Aswege Kaminyoge