Sibuka FM

Simiyu: Askari aliyejeruhi mwanae afikishwa mahakamani

17 February 2023, 1:48 pm

Picha ni Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Simiyu na Mahakama ya wilaya ya Bariadi

Askari wa jeshi la polisi mkoa wa Simiyu mwenye no H.4178 PC Abati Benedicto Nkalango miaka (27) aliyempiga  mwanae  mwenye miaka( 7) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika  shule ya Herbeth Gappa English Mediam  na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kisa cha kutokujua kusoma  amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kesi hiyo no 8 ya mwaka 2023  inayomkabili askari huyo imetajwa leo February 16, 2023 katika mahakama ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu , mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bariadi  Mhe.Mariam Nyangisi ,Mwendesha mashtaka wa serikali Daniel Masambu amesema mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa moja la kufanya ukatili dhidi ya mtoto ambaye alikuwa chini ya malezi yake.

Masambu amesema  mtuhumiwa huyo  ametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 169(A) kifungu kidogo  cha kwanza na cha pili cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022.

Aidha ameongeza kuwa Januari 15, 2023 mtuhumiwa alitenda ukatili kwa mtoto wake (7) jina linahifadhiwa kwa kumchapa sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha madogo na makubwa sehemu za mgongoni na masikioni.

Mara baada ya kusomewa shitaka mtuhumiwa alikana na wakakili wa serikali aliieleza mahakama kuwa upelelezi juu ya shauri hilo umekamilika na kuomba kutajiwa tarehe ya kuanza kusoma hoja za awali.

Kesi hiyo itaendelea tena March 2,2023 kwa  hoja za awali ambapo hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bariadi Mariam Nyangisi alimueleza mtuhumiwa kuwa dhamana ipo wazi.

Mtuhumiwa alishindwa kutimiza sharti la dhamana ambalo alitakiwa  kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho pamoja na bondi ya  shilingi milioni 3 na hivyo  kurejeshwa mahabusu.