Sibuka FM

TARURA KUJENGA BARABARA ZA LAMI MJINI MASWA

January 14, 2023, 4:54 pm

Na mwandishi wetu,Samuel Mwanga.

Wakala wa Barabara wa Mjini na Vijijini (TARURA)katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kujenga barabara za kiwango cha lami katika mitaa mitatu  mjini  Maswa katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Maswa,Mhandisi Francis Kuya wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mji wa Maswa kujionea kazi zilizofanywa na Tarura.

Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika kuboresha barabara za mitaa katika mji huo licha ya kujenga mitaro ya maji ya mvua kwa sasa watajenga barabara za kiwango cha lami katika mitaa ya Lubala,Kapilima na Ziota.

Mhandisi Kuya amesema kuwa gharama za ujenzi huo ni kiasi cha Sh Milioni 500 ambazo zinatokana na Mfuko wa Jimbo la Maswa Mashariki.

“Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia mfuko wa jimbo la Maswa mashariki tunategemea kupokea  kiasi cha milioni 500 pindi tu mwaka wa fedha utakapoanza ambazo zitaenda kuboresha miundombinu ya barabara mjini hapa ’’ amesema Francis Kuya

Amesema kuwa tayari Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hizo zenye urefu wa Kilomita moja amekwisha kupatikana na tayari ameanza kazi za awali ambazo ni pamoja na kuondoa mabomba ya maji,nguzo za umeme na kuondoa miamba ya mawe.

Tarura katika wilaya ya Maswa imekuwa ikipokea fedha toka serikali kuu kiasi cha Sh Bilioni 4.226 kwa mwaka kwa ajili ya kuboredha barabara za wilaya hiyo kwa mchanganuo wa Sh Bilioni 2 za matengenezo ya barabara zinazotokana na tozo za mafuta,Sh Bilioni moja za Mfuko wa majimbo mawili ya uchaguzi (jimbo la Maswa Mashariki sh. Milioni 500 na Jimbo la Maswa Magharibi Sh. Milioni 500) na Sh .Bilioni 1.226 zinazotokana na Mfuko wa barabara hapa nchini.