Sibuka FM

WANANCHI WILAYANI MASWA WAASWA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI.

27 July 2022, 11:41 am

Balozi  wa  Maji nchini  Mrisho  Mpoto maarufu  kwa  Jina  la  Mjomba  Amewaasa  Wananchi Wilayani  Maswa  Mkoani  Simiyu  kutunza  vyanzo   vya  Maji  likiwemo  Bwawa  la  New  Sola   lililopo  katika   kijiji  cha  Zanzui  kata  ya  Zanzui..

Balozi  Mpoto  ametoa   nasaha  hizo alipotembelea  Bwawa  hilo  ili  kijionea    Uhifadhi  wa   chanzo  hicho  kinachohudumia  Wananchi  wa  Mji  wa  Maswa  na  Vijiji  12   vinavyozunguka   Bwawa  hilo..

Amesema  kuwa   vyanzo  vya  Maji vilivyopo  katika maeneo  yetu  ni  Muhimu  kwani  vimekuwepo  miaka  mingi  na  kutunzwa  na  watu  mbalimbali  hadi  kufikia  hapa  hivyo  kila  mwananchi   anapaswa  kuendelea kuvilinda  na  kuvitunza  ili  viweze  kusaidia  Jamii  na  Vizazi  vijavyo..

“tutakapoingiza mifugo pale Ile mifugo itakwenda itakanyagakanyaka na ule udongo utalainika na kusababisha kina cha maji kupungua na tukiwa na mifugo mingi tukisema washambulie pale hatukai hata miezi sita maji yote yataisha lakini mifugo ile nyie mnajua tunaipeleka kwenye majosho inapigwa dawa na ng’ombe anywi maji ya mwanzoni anakunywa maji ya katikati akisogea pale ni kama anaoga na dawa yote inaishia kwenye maji… lakini hawa ng’ombe pia ninyi mnafahamu wanaweza kujisaidia pale kwahiyo maji yale yatachafuka na hivyo kuleta gharama kubwa ya kuyasafisha/ kuyatibu …lakini ng’ombe hao wanapoenda kunywa maji wanatengeneza njia na hivyo kusababisha maji kutoka na kupoteza muelekeo kwa hiyo hiki chanzo hakitakiwepo lakini ninyi mkaelilishana mkazungumza mkaona kwamba tunahitaji kukihifadhi hiki chanzo kiweze kutusaidia tena na tena niwapongeze sana ” amesema balozi Mpoto.

Aidha   Mkurugenzi  wa  Bodi  ya  Maji  ya  Bonde  la  Ziwa   Victoria  Dr  Renatus  Shinhu amesema   kuwa   ni  vyema  wakashirikiana  na  Wananchi  wa  Maeneo  yanayozunguka  Bwawa   hilo  katika  Utunzaji ,  Utambuzi  wa  maeneo   na  Uwekaji  wa  Vigingi  vya  Mipaka.

Dr  Shinhu  amesema  kuwa  Bwawa  hilo  ni  Muhimu  kwani  linategemewa  na  Wananchi  wengi  wa  Mji  wa  Maswa  hivyo  ni  Vizuri  kuheshimu   mipaka  yote   iliyowekwa  kuzunguka  Chanzo  hicho ili  kuepuka  Uchafuzi  wa  Mazingira   unaosababisha  kukauka  kwa  Bwawa   hilo..

Nandi  Mathias  ni   Mkurugenzi Mtendaji  wa   Mamlaka  ya  Maji na  Usafi wa  Mazingira  Maswa-MAUWASA  amesema  kuwa  Mradi  huo  umepunguza  Magonjwa ya  Matumbo  na  Kuhara  hivyo  wananchi  kujikita  katika  Uazilishaji  na  kujiongezea  Kiapato..

Nandi  Mathias  amesema  kwa  sasa  Ushirikiano  Umeongezeka  kati  ya  Mauwasa  na  Wananchi  wanaozunguka  Chanzo  hicho  cha  Maji  hali  inayopelekea  Wananchi  kuwa  Sehemu  ya  Ulinzi  wa  Bwawa  hilo..

Mbuke John ni mkazi wa kijiji cha Zanzui amesema bwawa hilo limekuwa msaada kwa wananchi kupata maji safi na salama huku mwenyekiti wa kijiji cha Mwabayanda Cosmas Kija akiomba ushirikishwaji wa wafugaji katika utunzaji uendelee sambamba na kufanya tathimini kutokana na idadi ya watumiaji kuongezeka .