

September 9, 2021, 1:20 pm
Mtoto mwenye umri wa miaka 5 anayejulikana kwa jina la Masule. S. Cosmas mkazi wa kijiji cha zawa kata ya mwanghonori wilayani Maswa Mkoani Simiyu amefariki baada ya kujeruhiwa na fisi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Tukio hilo limetokea Siku ya Jumatano tarehe 8.9.2021 majira ya saa 15:00 alasiri.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Richard Abwao amesema kuwa tukio hilo limetokea wakati mtoto huyo akiwa na wenzake ambao ni Naomi Amosi na Scholastika Wahumija,
Wakiwa wanachunga ng`ombe na mbuzi kwenye maeneo ambayo yapo mbali na makazi yao, ndipo fisi huyo alitokea na kuanza kuwakimbiza na kufanikiwa kumkamata Mtoto huyo Masule Cosmas na kuanza kumshambulia baadhi ya viungo vya mwili ambavyo ni shavu la kulia na kumtoa ngozi ya kichwa pamoja na macho yote mawili kitendo kilichopelekea kifo chake.
Jitihada za kumtafuta fisi huyo zilifanywa na wananchi na kufanikiwa kumpata na kumuua.
Mwili wa Marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na baadaye kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Jeshi la polisi Mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto wao dhidi ya wanyama wakali kwenye maeneo yao hasa vijijini.