Sibuka FM

Ded Maswa hakuna upungufu wa panadol kama inavyosambaa katika mitandao ya kijamii

17 July 2021, 5:18 pm

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Dr.Fredrick Sagamiko amewaomba watanzania kupuuza taarifa ambayo inasambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya ukosefu wa dawa aina ya Panadol katika hospitali ya wilaya ya Maswa .

Taarifa ya kutokupatikana kwa dawa aina ya Panadol iliibuliwa na mmoja wa wananchi wakati wa mkutano wa hadhara na mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila wenye lengo la kujitambulisha na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi uliofanyika mnamo July .14 katika viwanja vya Madeco wilayani hapo ambapo mwananchi huyo alilalamikia ubovu wa huduma za afya katika hospitali ya wilaya hiyo ikiwemo ukosefu wa Panadol.

Kwenye picha ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa Dr.Fredrick Sagamiko

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Maswa Dr.Fredrick Sagamiko amesema kuwa kimsingi taarifa hiyo siyo ya kweli hivyo wananchi waipuuze kwani hali ya upatikanaji wa dawa zinazofatiliwa na serikali(dawa muhimu) ikiwemo na dawa aina ya Panadol inayolalamikiwa kutokuwepo  hospitalini hapo ipo tena za aina mbili ya Kidonge na Maji.

Sauti ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa Dr.Fredrick Sagamiko

Kufuatia sintofahamu hiyo Dr.Sagamiko ametumia mkutano huo wa waandishi wa habari  kutoa wito kwa wanahabari kutumia vizuri kalamu zao katika kuhabarisha watanzania na kuongeza kuwa sekta ya habari ni wadau muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu .

Sauti ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa Dr.Fredrick Sagamiko

James Bwire ni mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Maswa amesema kimsingi dawa zinazofatiliwa na serikali(dawa muhimu) hali ya upatikanaji wake ni asilimia mia moja na kuongeza kuwa pale kunapokuwa na sintofahamu  juu ya utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo  wananchi wapeleke malalamiko yao katika dawati la malalamiko ambalo lipo chini ya afisa ustawi wa jamii.

Sauti ya mganga mfawidhi hospitali ya wilaya ya Maswa James Bwire

Awali kabla ya kuanza kuzungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa wilaya hiyo Dr.Sagamiko alitoa nafasi kwa waandishi wa habari kutembelea store ya dawa kwa lengo la kujionea uhalisia wa taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii iliyochapishwa na chombo kimoja cha habari hapa nchini kuhusu ukosefu wa dawa aina ya Panadol.