Shirika la CLWF kutoka Korea laanza kujenga Madarasa Sengerema
18 May 2024, 7:42 pm
Shule ya Msingi Isole iliyopo kata ya Buyagu Halmashauri ya Sengerema imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa muda mrefu, hali iliyopelekea shirika la CLWF kujitolea kujenga vyumba vinne vya madarasa shuleni hapo.
Na;Emmanuel Twimanye
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Christian Life World Mission Frontiers kutoka nchini Korea Kusini limeanzisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya Msingi Isole iliyopo Kata ya Buyagu Wilayani Sengerema ili kutatua changamoto ya mlundikano wa wanafunzi Darasani .
Akizindua ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa vinavyotarajia kugahrimu Zaidi ya shilingi milioni 40 Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Tanzania Joshua John amesema kuwa wameamua kutoa msaada huo ili kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta ya elimu.
Makamu wa Rais wa shirika hilo Methew Lubongeja amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kusababisha kupata ujauzito na kukatisha ndoto zao za kielimu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo na baadhi ya viongozi wa kata hiyo pamoja na kushukuru shirika hilo kwa msaada huo wameahidi kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamesema kuwa wamekuwa wanasoma wakiwa wamelundikana Darasani hivyo utakapokamilika ujenzi wa madarasa hayo itasaidia kusoma katika mazingira rafiki sambamba na kuongeza ufaulu.