Sengerema FM

Tanzania kuzidi kuwawezesha wanawake kimaendeleo.

21 October 2021, 1:20 pm

Tanzania imeazimia kuendelea kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika Uongozi na uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kupitia Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Mwajuma Magwiza wakati akizungumza namna Tanzania ilivyojifunza kutokana na Mkutano huo wa Wanawake nchini Urusi.

Bi. Mwajuma amesema kuwa Tanzania imejifunza kuwa Wanawake wanaweza kushiriki katika Sekta mbalimbali na kutoa mchango wao katika Sekta husika na kutumia fursa hizo kupata ajira na kuajiri wengine.

Ameongeza kuwa Tanzania inahimiza Wanawake kushiriki katika uchumi wa viwanda ila kutokana na Mkutano huo imeleta changamoto mpya za kuangalia maneno ambayo Wanawake wanaweza kushiriki katika kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni sanaa ya uigizaji, ulimbwende na michezo ambapo Wanawake wanaweza kushiriki vizuri iwapo kutakuwa na mazingira mazuri yanayoweza kuwa na tija katika maendeleo yao na Taifa kwa ujumla

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imeshaanza na inaendelea kuwawezesha wanawake katika Uongozi na majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi yameanzishwa katika ngazi za Wilaya na Mkoa ili kuweza kuwapa fursa katika Sekta mbalimbali.

Tanzania imeshiriki katika Mkutano wa Tatu wa Wanawake nchini Urusi uliofanyika nchini humo kuanzia tarehe 13-15 Oktoba 2021 ambapo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt Dorothy Gwajima alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

mkurugezi idara ya maendeleo ya jinsia Bi mwajuma magwiza