Sengerema FM

Rais Samia afanya uteuzi, Sabaya pembeni kupisha uchunguzi.

13 May 2021, 11:27 pm

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan amemsimamisha kazi mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Taarifa iliyotolewa Alhamisi Mei 13, 2021 na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Sabaya amesimamishwa kazi kuanzia leo.

Sabaya aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo na Hayati John Magufuli Julai 28, 2018.

Mbali na kumsimamisha Sabaya, taarifa hiyo inaeleza kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi ameteua watendaji mbalimbali.

Inaeleza kuwa rais amemteua Nsubili Joshua kuwa karani wa baraza la mawaziri, ambapo hapo awali Joshua alikuwa akikaimu nafasi hiyo. Pia amemteua Ayub Makoye kuwa naibu karani wa baraza la mawaziri, Makoye alikuwa akikaimu nafasi hiyo.

Pia rais Amemteua Dk  Stergomena Tax kuwa mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya uongozi. Dk Tax ni katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Amemteua Dk Laurian Ndumbaro kuwa makamu mwenyekiti wa taasisi ya uongozi. Dk  Ndumbaro ni katibu mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Inaeleza kuwa Rais Samia pia amefanya uteuzi wa wajumbe wa bodi ya taasisi ya uongozi ambao ni Balozi Riitta Swan, Profesa Penina Mlama, Lina Soiri, David Walker,  Suzan Mlawi, Dk  Hamis Mwinyimvua na Profesa Samwel Wangwe na wote uteuzi wao umeanza leo isipokuwa kwa Ishmael Kasekwa aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Uteuzi wa Kasekwa ulianza Mei 10, 2021 akichukua nafasi ya Dk Rosebud Kurwijila ambaye amemaliza muda wake.