Sengerema FM

SERIKALI YASITISHA BEI MPYA ZA VIFURUSHI VYA INTANETI

3 April 2021, 8:34 am

Taarifa iliyotolewa na Tcra kwa umma

Kufatia malalamiko ya baadhi ya watumiaji wa mitandao ya Internet Nchini,baada ya kutangazwa kwa bei mpya za vifurushi, Serikali imetangaza kusitisha kutumika kwa gharama hizo hadi hapo itakapotangazwa baadaye.

Uamuzi huo ni habari njema kwa watumiaji wa mitandao ya simu ambao, tangu kutangazwa kwa bei hizo mpya mapema Ijumaa ya Aprili 2, 2021, wamekuwa kwenye mjadala mzito kwani, matarajio ya wengi ilikuwa ni kushuka kwa gharama hizo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, amesema matumizi ya bei mpya ya vifurushi yamesitishwa kwa muda.

Hata hivyo, amesema uamuzi huo utahusu vifurushi vya data pekee huku vile vya ujumbe mfupi wa maneno na kupiga zitaendelea kama ilivyotangazwa.

Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na TCRA, zimeanza kutumika 02/04 mwaka huu ambapo, matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini ikawa tofauti.