Radio Jamii Kilosa

Kata ya malolo yapongezwa kwa ujenzi wa kituo Cha Afya .

21 April 2021, 10:15 am

Wananchi wa kata ya Malolo pamoja na uongozi wake wamepongezwa kwa namna ambavyo wameonyesha umoja na ushirikiano katika kujiletea maendeleo katika kata yao kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kufanikisha ujenzi wa kituo cha afya Malol.

Viongozi wa Kamati ya fedha Uongozi na Mipango wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa pamoja na Viongozi wa kata ya Malolo wakiwa katika ziara ya ukaguzi wa Mradi wa ujenzi Kituo cha Afya Malolo .

Pongezi hizo zimetolewa Aprili 20 mwaka huu na Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ilipotembelea kituo hicho katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi namna kilivyofanikisha ujenzi wa majengo mbalimbali ya kutolea huduma za afya ikiwemo jengo la maabara,  mapokezi na jengo pacha la mama na mtoto ambalo ndani yake zitapatikana huduma za upasuaji.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh.Wilfred Sumari

Akitoa pongezi zake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Wilfred Sumari amesema kituo hicho ni cha mfano wa kuigwa kwani kazi iliyofanyika ni kubwa ambapo hadi sasa imefikia asilimia 95 pia ameutaka uongozi wa Halmashauri kuwasiliana na RUWASA ili kutatua changamoto ya maji inayoikumba kata hiyo huku akizitaka kata nyingine kuiga mfano wa kata ya Malolo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za jamii Mh. Meshack Munyi licha ya kupongeza kazi iliyofanyika katika kituo hicho amewataka kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwa kuongeza kasi ya kujiletea maendeleo pamoja na kuhakikisha wanahimizana katika suala la elimu ili kila mtoto anayestahili kupata elimu apate elimu.

 Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya ya Kilosa Francis Kaunda amesema kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na kata hiyo na kuiwezesha kifedha ili kuhakikisha kituo hicho kinamalizika na kuanza huduma mara moja huku akisema kuwa changamoto ya upatikanaji wa maji ameichukua na itafanyiwa kazi.