Radio Jamii Kilosa

Halmashauri ongezeni nguvu katika sekta ya kilimo-DC Mgoyi.

11 March 2021, 7:52 pm

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam I Mgoyi .

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya  Kilosa kutambua kuwa Wilaya ya Kilosa ni wilaya ya kilimo iliyojaa mito yenye maji ya kutosha hivyo ni vema wilaya ikajikita zaidi katika uzalishaji ili kupata mazao ambayo yatapelekwa kiwandani huku akitaka Halmashauri kupanga bajeti ya kutosha upande wa kilimo na kuwekeza zaidi katika kilimo ili kupata tija zaidi.

Mgoyi amesema kwa sasa wilaya imekuwa ikipanda kiwango cha uzalishaji hali inayoonyesha kuongezeka kwa maeneo ya kulima huku migogoro ya wakulima na wafugaji ikipungua na kupelekea wananchi kuweza kulima na kuvuna huku akisema kuwa wakulima wanahitaji zaidi huduma za ugani kwa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana ili kuzalisha kiwango kinachotarajjiwa .

Pamoja na hayo amesisitiza kuwepo kwa mashamba darasa ya kijiji kwa kila kijiji kwani mashamba hayo yatasaidia wananchi kujifunza namna ya kilimo bora halikadhalika namna ya kuhifadhi mazao yao baada ya kuvuna kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya kuhifadhi mazao ambayo kwa asilimia kubwa mengi yamekuwa yakitunzwa katika namna isiyo sahihi na kupelekea upotevu wa mazao sambamba upatikanaji wa vifaa vya kuhifadhia mazao.

Aidha ametoa wito kwa MVIWATA licha ya kufanya mambo mazuri amewata kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na semina nyingi zaidi kwa wakulima lengo ikiwa ni kuwasaidia wakulima katika kuongeza ujuzi na hamasa kwa wakulima ili waweze kupiga hatua zaidi na kukuza uchumi wao kwani wanahitaji zaidi kujengewa uwezo na kwamba Serikali iliyopo madaraka imejikita zaidi katika kutetea wanyonge. 

Naye Mratibu wa MVIWATA Morogoro Joseph Sengasenga amesema MVIWATA inashirikiana na Halmashauri kwa kufanya mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ujasiriamali wa aina mbalimbali, kuzalisha kwa tija lakini pia ina mpango wa kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya wakulima ili waweze kujifunza zaidi na kwamba inatekeleza shughuli zake kwa kushirikiana na Halmashauri kwani wanufaika wa shughuli mbalimbali zinazofanywa  ni kwa faida ya wakulima na wananchi kiujumla.