Radio Jamii Kilosa

Prof Kabudi aongeza nguvu ujenzi shule za sekondari Dakawa mazoezi,Magole na Dumila kwa mifuko 450 ya saruji.

1 February 2021, 10:28 am

Mbunge wa jimbo la Kilosa akikabidhi mifuko ya saruji kusaidioa ujenzi was vyumba vya madarasa .

Mbunge wa Jimbo la Kilosa Paramagamba Kabudi Januari 31 amekabidhi mifuko 450 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 7.2 ikiwa ni fedha zake binafsi katika shule za sekondari Mazoezi Dakawa, Magole na Dumila ambapo kila shule imepata mifuko 150 kwa ajili ya kuzipa nguvu ziweze kumaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Akizungumza wakati akikabidhi mifuko hiyo akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale na timu yake amesema kuwa mifuko hiyo ya saruji itasaidia kumaliza ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi mbili za shule ya Sekondari Magole shule ya Mazoezi Dawaka pamoja na vyumba vinne vya madarasa katika shule ya Sekondari Dumila.

Amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutaweza kutatua changamoto zilizopo za upungufu wa vyumba vya madarasa hivyo kuwezesha watoto waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kuanza masomo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza cha kwanza lazima wasome.

Mkugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa Asaijile Mwambambale akizungumza jambo na Mbunge wa Jimbo la Kilosa Prof Kabudi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale amemshukuru Mh Kabudi kwa kujitoa na kuchangia maendeleo kwa fedha zake binafsi na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Mbunge pamoja na Serikali kwa ujumla katika kutatua changamoto za elimu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande mwingine Mwambambale amesema kiwango cha ufaulu kimeongezeka na kuwezesha Halmashauri ya Kilosa kushika nafasi ya nne kimkoa kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka mwaka huu.