Radio Fadhila

DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba aiwaza Al Merrikh

28 Febuari 2021, 4:16 mu

DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba amesema kuwa mchezo wake ujao dhidi ya Al Merrikh utakuwa mgumu tofauti na wengi wanavyofikiria.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ikiwa ipo kundi A ipo nafasi ya kwanza na ina pointi sita, mechi zake zote mbili imeshinda.

Ilianza kushinda ugenini mbele ya AS Vita 0-1 Simba kisha ikashinda bao 1-0 dhidi ya Al Ahly, Uwanja wa Mkapa.

Mchezo wake unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika itakuwa Machi 5, ugenini nchini Sudani, timu hiyo ilikuwa mikononi mwa Gomes kabla ya kuibukia ndani ya Simba Januari 24 kuchukua mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye yupo zake Morocco.

Gomes amesema:”Kuhusu hilo tuna muda mwingi wa kufikiria juu ya mechi ijayo, itakuwa mechi ngumu kwa sababu naijua hiyo timu. Lakini kwa sasa nadhani tunatakiwa kutojipa mawazo sana kuhusiana na mechi hiyo inayokuja.

“Wachezaji wanajua kwamba tunahitaji ushindi ila inahitaji muda na tutapambana ili kupata matokeo chanya ndani ya uwanja, kikubwa sapoti pamoja na umakini kwani kuna kazi kubwa ya kufanya,”.