Radio Fadhila

Waarabu wapigiwa hesabu kali na Simba kwa Mkapa

19 Febuari 2021, 10:14 mu

 SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Simba, amesema kuwa wapinzani wao wote ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa pamoja na Al Ahly wameandaliwa dozi zao pale watakapokutana ndani ya uwanja.

Simba ikiwa Kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukusanya pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita, ina kazi ya kusaka pointi tatu dhidi ya Al Ahly,inayoongoza kundi hilo kwa idadi ya mabao matatu huku Simba ikiwa na bao moja ipo nafasi ya pili na zote zina pointi tatu.

Mchezo huo utachezwa Uwanja wa Mkapa, Jumanne, Februari 23 na unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo, wana kumbukumbu ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Waarabu hao wa Misri walipokutana kwenye mchezo wa hatua ya makundi, msimu wa 2018/19, Uwanja wa Mkapa, Dar, Februari 19, 2019.

Al Ahly watawafuata Simba wakiwa na hasira za kulipa kisasi cha kufungwa kwa bao la Meddie Kagere.

Matola amesema kuwa wachezaji wao waliopo wanatambua namna kundi lilivyo pamoja na ushindani jambo litakalowafanya waingie uwanjani kupambana bila kuogopa.

“Kundi lipo wazi kwamba ni gumu, sasa hapo wachezaji mtihani wao ni kufaulu kwa kupata ushindi ndani ya uwanja kwa kila timu ambayo tutakutana nayo bila kujali kwamba ni Al Ahly ama AS Vita, mashabiki watupe sapoti,” amesema Matola.