Pangani FM

Suluhisho la migogoro ya Ardhi na uharibifu wa mazingira Pangani

10 February 2023, 10:37 am

Mmoja wa wanakamati wa Mazingira wa kijiji cha Kwakibuyu akwasilisha hoja juu ya utunzaji wa vyanzo vya Maji. Picha na Erick Mallya

Katika ngazi ya kijiji mamlaka inayohusika na maandalizi ya mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji ni halmashauri ya Kijiji ambayo inaweza kufanya utekelezaji wake kupitia kamati ya usimamizi na matumizi ya ardhi.

Na Erick Mallya

Serikali ya kijiji cha Kwakibuyu wilayani pangani Mkoani Tanga imetakiwa kutengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kusaidia katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji unaotokana na ufugaji holela.

Hayo yamejiri wakati wa mafunzo ya kuzijengea uwezo kamati za mazingira wilayani Pangani mkoani Tanga ili kuweza kuhusisha masuala ya jinsia katika mipango kazi yao, yanayoendela katika kijiji hicho.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya  mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani Bwana Daudi Mlahagwa amesema kuwa kwa sasa kijiji hicho hakina mpango rasmi wa matumizi bora ya ardhi hali inayopelekea ugumu katika kutatua changamoto mbalimbali za matumii ya Ardhi.

Mkiwa na ule mpango utauruhusu kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli ambazo wananchi wenu wanazifanya kama hapa hamtaki kuwa na mifugo basi hamtengi eneo kwa ajili ya mifugo ina maana wakiingia wafugaj mtawaambia kuwa hamna eneo kwa ajili ya mifugo ndio uzuri wa mpango hivyo atakayeingia atalazimika kwenda sehemu nyingine ambazo zina mpango wa matumzi bora ya ardhi yenye eneo la ufugaji kama Mburizaga, Sange, stahabu au Bushiri na Mkalamo hapa hatokaa

Amesema Bwana Mlahagwa.

Mkuu wa Idara ya Mazingira Halamashauri ya Wilaya Pagani Bw. Daudi Mlahagwa Akisisitiza jambo katika mafunzo hayo. Picha na Erick Mallya

Awali wakati wa majadiliano ya namna bora yakulinda rasilimali za mazingira zilizopo katika kijiji hicho baadhi ya wajumbe hao walilalamikia ufugaji holela kama chanzo cha uharibifu wa mazingira ikiwamo vyanzo vya maji na kueleza kuwa hali hiyo imesababisha vurugu na uvunjwaji wa Amani.

Mwezeshaji kutoka shirika la UZIWKASA akifafanua jambo kwa baadhi ya wanakamati hao wakati wa kutengeneza mipango kazi yao.

Naye Mwezeshaji kutoka shirika la UZIKWASA bwana Nickson Lutenda amesisitiza uwepo wa mpango huo ili kuwezesha wadau wengine kusaidia upatikanaji wa haki pale migogoro inapotokea katika kijiji hicho.

Sheria zile zitawalinda na hata kuwarahisishia maafisa katika kijiji chenu kuchukua hatua dhidi ya uharibifu unaotokana na matumizi holela ya ardhi, inawezekana mlikuwa manchukulia kitu hiki kama masiahara lakini sasa inabidi muonyeshe nia ili iwe rahisi kusaidiwa

Amesema Bwana Nickson Lutenda

Baadhi ya wanakamati wa Kwakibuyu wakijadiliana katika kutengeneza mipango kazi yao.

Kufuatia hayo Mtendaji wa Kata ya Kipumbwi bwana Omari Akida amesema kuwa anatambua changamoto hiyo na kuahidi kuishughulka mara tu baada ya mafunzo hayo.

Kitu tulichogundua pia kero ya wafugaji na wakulima ambapo bila ya kuanzisha mipango ya matumizi bora ya ardhi hatuwezi tukafanikiwa kilichopo mbele yangu baada ya mafunzo haya kwa kushirikiana na kamati yangu ni kuanzisha mpango huo ili kuondoa kero na muigiliano.

Amesema Bwana Omari Akida Mtendaji wa Kijiji hicho.

Kwa mujibu wa kijarida haki ardhi cha kuielimisha jamii juu ya masuala muhimu ya haki za ardhi kuhusu uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji toleo la 5 Julai mwaka 2020

Katika ngazi ya kijiji mamlaka inayohusika na maandalizi ya mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji ni halmashauri ya Kijiji ambayo inaweza kufanya utekelezaji wake kupitia kamati ya usimamizi na matumizi ya ardhi.

Jambo la msingi katika ngazi ya kijiji  ni kuzingatia kuwa, mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji ni matokeo ya mchakato shirikishi ambao bila kufuata hatua zinazotakiwa utakosa uhalali wake na hasa pale wananchi wanapokuwa hawakushiriki kikamilifu kama mwananchi mmoja mmoja au kupitia mikutano yao mikuu ya vijiji.

Hayo yamejiri katika mafunzo yanayolenga kuzijengea uwezo kamati za mazingira wilayani Pangani ili kuweza kuhusisha masuala ya jinsia katika mipango kazi yao, mafunzo yanayotolewa na Shirika la UZIKWASA lililopo wlayani Pangan kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya hiyo.

Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoanza Februari 7 yanatarajiwa kukamilika Ijumaa februari 9.