Pangani FM

Mguso kwa Watumishi wapya Pangani.

22 November 2022, 4:35 pm

Watumishi wa kada mbalimbali za Halmashauri ya wilaya ya Pangani waloshiriki kwenye mafunzo ya Siku tatu ya uongozi wa mguso yanayotolewa na Shirika la UZIKWASA wamelishukuru shirika hilo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma pamoja na uongozi wao.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ofisi mpya za Shirika la UZIKWASA zilizopo katika kijiji cha Boza wilayani Pangani Mkoani Tanga.

Sehemu kubwa ya watumishi hao ni wapya katika idara za Halmashauri hiyo ambao walikuwa bado hawajapatiwa mafunzo ya mguso.
Kupitia afua mbalimbali za Shirika la UZIKWASA watumishi, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii wamepatiwa mafunzo ya mguso kuanzia ngazi ya kjiji mpaka wilaya.

Bi Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya wilaya Pangani Bi. Sekela Mwalukasa ameeleza kuwa mafunzo ya mguso yanatumia mbinu mbalimbali ambazo anaamini zitamsaidia kiongozi katika majukumu yake.
“UZIKWASA wana mbinu mbalimbali kwenye mafunzo haya ya mguso na kama kiongozi lazima uwe mfano wa kuigwa hivyo kupitia mbinu hizi za kiuwezeshaji jamii ya pangani itakuwa na mabadiliko mazuri na pangani itapata maendeleo” – Amesema Bi. Sekela

Mwezeshaji kutoka Shrika la UZIKWASA Bi. Salvata Kalanga ameeleza akielezea umuhimu wa mafunzo hayo ametoa wito kwa watumishi hao kuendelea kutathmini nafasi zao katika kuleta maendeleo endelevu Pangani baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

“mafunzo ya uongozi wa mguso yanamsaidia kiongozi kujua wajibu wake kwa anaowaongoza na yanamjenga kiongozi kujitafakari na kujitathmini ili kujua ni mambo gani anapaswa kufanya na kuleta mabadiliko kwake na kwa wale anaowaongoza,tayari mafunzo haya yameshawafikia viongozi mbalimbali hapa wilayani pangani kuanzia ngazi ya kijiji,kata,wilaya mpaka mkoa, na mafunzo haya ukiyafuatilia kama kiongozi utaona mabadiliko tu kwa jamii.”- Amesema Bi. Salvata.