Mzinga wa Nyuki
Pangani FM

Wagawa Mizinga 40 ya Nyuki Pangani

25 October 2022, 12:18 pm

Taasisi ya Foundation for Trees Tanzania iliyopo Jijini Tanga  imetoa Mizinga 40 ya Nyuki kwa Kikundi cha Ufugaji Nyuki cha MSETO kilichopo Wilayani Pangani ili kuwezesha wananchi hao kufanya shughuli za ufugaji na kuachana na uharibifu wa Mazingira.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa mizinga hiyo  iliyofanyika Nov 24 katika Kijiji cha Pangani Magharibi, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Bwana Emmanuel Swai amesema sababu kubwa za uharibifu wa mazingira zinatokana na kipato duni hivyo mizinga hiyo itasaidia kuboresha kipato cha watu na hatimaye kupunguza uharibifu.

Baadhi ya wanakikundi waliopatiwa mizinga ya Nyuki.

Bwana Swai amewahakikishia wanakikundi hao kuwa Taasisi hiyo itakuwa ni sehemu ya soko la asali na kuwataka kuwa mfano mzuri katika kutekeleza mradi huo ili kuwanufaisha wananchi wa Pangani kiuchumi na kimazingira.

Pangani FM imezungumza pia na baadhi ya wanakikundi  hao ambao mbali na kuishukuru Taasisi ya foundation for trees Tanzania wamesema ni wakati sasa kwa wao kujikwamua kiuchumi kupitia ufugaji nyuki na kuahidi kuiendeleza mizinga hiyo.

Naye Afisa Maliasili na Mazingira Wilaya ya Pangani Bwana Twahiru Mkongo amesema Halmashuri ipo tayari kushirikiana na wanakikundi hao ili mazao ya nyuki yawasidie katika kujiingizia kipato.

Ugawaji wa mizinga ya nyuki unatokana na utekelezaji wa mradi wa uchumi wa Bluu katika hifadhi ya bahari Tanga –Pemba unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland na kusimamiwa na Shirika la IUCN Tanzania na taasisi ya Foundation For Trees Tanzania inasimamia upandaji wa miti.