Pangani FM

Watu Nane wa Familia Moja wahisiwa kula chakula chenye Sumu Pangani.

17 August 2022, 4:04 pm

 

Hali ya afya ya watu wa familia moja waliopata madhara baada ya kula chakula kinachohisiwa kuwa kimechanganyika na sumu wilayani Pangani Mkoani Tanga inaendelea vizuri na tayari  saba kati yao  wameruhusiwa kutoka hospitalini huku  mmoja akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.

Hayo yamesemwa na mganga mfawidhi wa hosiptali ya halmashauri ya wilaya ya Pangani Dr Hassan Msafiri wakati alipozungumza na Pangani FM akiwa hospitalini hapo.

“Jumla tulikuwa na wagonjwa nane, sasa hivi wodini ambebaki mmoja tu wengine wameruhusiwa, huyu mmoja alikuja katikahali ambayo haikuwa nzuri alikuwa ahawezi kujitambua lakini sasa hivi anaweza kujitambua na hali yake inazidi kuimarika” Amesema Dk.Hassan Msafiri.

Dr. Haasan amesema kuwa  wanaendelea na uchunguzi kubaini kisababishi cha madhara hayo ikiwemo chanzo kinachowea kuwa kimepelekea kuzalisha sumu.

wale wagonjwa wote walikula chakula kimoja na wakapata haya matatizo, kwenye uchunguzi wetu wa awali unasema kwamba kitaalamu unaweza kula chakula kikashikwa na sumu, sumu inaweza kuwa imezalishwa kutokana labda na uhifadhi wa chakula labda kilikuwa kimelala na wakati wa kuhifadhi labda mazingira hayakuwa mazuri, yakazalisha bakteria na wakasababisha madhara au wakati wa kutengeneza kiliingiwa na Bakteria na wakasababisha madhara.” – Amesema Dk Hassani Msafiri

Hata hivyo  Dr Hassan amebainisha kuwa hali ya athari na muda wa kujitokeza mara baada ya mtu kula chakula chenye sumu inaweza kutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine kulingana na uwezo wa kinga za miili yao.

Kufuatia tukio hilo Dr Hassan ametoa wito kwa watu kuhakikisha usalama wa chakula chao kabla ya kula pamoja na kuzingatia njia sahihi za uhifadhi wa chakula.

Tukio hilo la familia ya watu nane kula chakula kinachohisiwa kuwa na sumu limetokea siku ya jumamosi august 13 mwaka huu katika kijiji cha Pangani Magharibi kilichopo wilayani Pangani Mkoani Tanga.