Pangani FM

Funguni Sekondari yapokea Milioni Mia Mbili za Mabweni.

26 July 2022, 6:55 pm

Shule ya Sekondari Funguni iliyopo Wilayani Pangani mkoani Tanga imepokea kiasi cha pesa shilingi millioni mia mbili  kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wakike na wakiume.

Akizungumza na Pangni FM katibu tawala Wilaya ya Pangani Mwalimu Hassani Nyange   ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ambayo amedai kuwa yatasaidia kupunguza vitendo vya utoro na kuwa na mchango mkubwa katika kunyanyua elimua ya Sekondari Pangani.

“Tumekuja kupokea taarifa juu ya fedha zilizoingia juzi Funguni Sekondari shilingi milioni mia mbili kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli mbili moja ya watoto wa kiume nyingine ya watoto wa kike, tunaishukuru sana serikali yetu pamoja na Mheshimiwa Aweso ,Mbunge wa Jimbo la Pangani ambaye amekuwa mpiganaji mkubwa kuhakikisha ndoto hii inatimia, katika shule hii tumekuwa tukihitaji Hosteli ili shule ifanye vizuri zaidi. Shule yetu hii ndiyo shule yetu ya Kata Pangani ambayo inafanya vizuri zaidi na katika moja ya mikakati ya walimu walisema tukipata Hosteli wanafunzi wakikaa hapa hapa watafanya vizuri zaidi”

-Amesema Mwalimu Nyange.

Aidha mwalimu Nyange amesema kuwa ujenzi huo unatakiwa kuanza na kukamilika kwa wakati ili kufikia lengo lililokusudiwa na serikali.

kwa mujibu wa Mwalimu Nyange mkakati uliopo kwa ajili ya  ujenzi wa mabweni hayo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi waliopo kidato cha tatu mwaka 2022 wanatumia mabweni hayo pindi watakapokuwa kidato cha nne mwakani.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw. Nasoro Gamba ameishukuru serikali kwa ujio wa pesa hizo ambazo na kueleza kuwa mradi huo utawezesha kufikia malengo yao kama shule na hatimaye kufanya vyema zaidi katika ufaulu.