Pangani FM

Wenye Ualbino waeleza matarajio yao kwenye Bajeti ya 2022/2023

14 June 2022, 1:38 pm

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba leo anatarajiwa kuwasilisha bungeni bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 41 sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti inayomalizika ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Bajeti ya serikali iliyoidhinishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ilikuwa shilingi trilioni 37.9 ambapo kati ya fedha hizo shilingi trilioni 23 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 14.9 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Kila Juni 13 dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino. Kufuatia hilo Pangani FM imezungumza na mwenyekiti wa chama cha Chama cha wenye ualbino Mkoani Tanga bwana Nuru Shekibula ili kujua matarajio yao katika Bajeti hiyo.

Mwenyekiti huyo akizungumza kutokea Mkoani Kagera ambapo ndipo maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa amesema kuwa kama chama wanategemea kupungua kwa gharama mbalimbali zitakazosaidia uendeshwaji wa chama chao pamoja na bidhaa nyingine zinazorahisisha shughuli zao za kila siku.

Pia mwenyekiti huyo amewahimiza watu wenye ualbino na wazazi wenye watoto wenye Ualbino kujitokeza kwenye zoezi la Sensa ambalo litafanyika mnamo mwezi wa nane ili kupata idadi itakayosaidia serikali kuwajumuisha kwa urahisi kwenye mipango yake.