Pangani FM

DC PANGANI alia na mimba likizo ya Corona.

8 March 2021, 8:14 pm

Ikiwa leo Ulimwengu unaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Wanawake Wilayani Pangani Mkoani Tanga wameaswa kujizatiti kwenye Malezi ya Watoto wao hasa wa kike ili kufikia lengo la Dunia yenye Usawa.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Funguni hapa Mjini Pangani.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah Issa ambaye ndiye Mgeni rasmi katika sherehe hizo, katika hotuba yake amesema ili kufikia dunia yenye usawa, wanawake ni lazima wajizatiti katika malezi yao hasa kwa watoto wa kike.

“Leo ni Siku ya Wanawake, na kauli mbiu ya mwaka huu tumeambiwa Wanawake kwenye Uongozi chachu katika kufikia usawa kwenye dunia. Uongozi unaanzia kwenye ngazi ya familia na kwenye familia kiongozi ni mama, lakini kina mama wenzangu naomba niseme kwa masikitiko makubwa sana, mwaka jana baada ya likizo ya Corona mpaka January mwaka huu mimba za mashuleni hazipungui 20” Amesema Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa “Tumekaa vikao tukapata majibu kwamba haya yamechangiwa na malezi”.“Wazazi wenzangu malezi yetu ndiyo yatakayo wafanya watoto wenu wafika kama nilipo mimi au hata zaidi”.

Aidha Bi. Zainab amewataka wazazi kuyapa kipaumbele masuala ya elimu kwa watoto wao katika masuala ya chakula kwa wanafunzi na kuzuia uzururaji hovyo wa watoto.

“Mtoto yeyote baada ya saa 12 jioni akikutwa barabarani, kwenye vigodoro yeye na mzazi wake watakaa ndani, kwahiyo wazazi tunawaomba muwasimamie watoto wasizurure hovyo mitaani”.Amesema Bi. Zainab na kuongeza kuwa “Mzazi ambaye atagoma kuchangia suala la chakula shuleni huyo naye tutampeleka mahakamani, maana haiwezekani kwenye harusi mnafanya wiki nzima lakini chakula cha mtoto shuleni mzazi anakwambia hela hana”

Amesema Bi Zainab Abdallah

Kuhusiana ushahidi hasa katika kesi za ukatili, Bi. Zainab amesema kesi nyingi zinakwama na washukiwa wa ukatili kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi uliokamilika, hivyo amewataka wazazi kutowaficha wahalifu kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli.

“Mnatulaumu sisi viongozi wa Serikali kwamba kesi hizi watu wanaachiliwa, tumekaa kikao cha kamati ya maadili ya mahakama na kufuatilia, tumegundua sababu kubwa ni kwamba watuhumiwa wanapoteza ushahidi, leo mtoto amebakwa ametishwa na mzazi akifika mahakamani anamtaja mwingine, tena wanataja watu ambao sio wa kazi wa hapa, mashahidi tunawatorosha kwenda Dar au Zanzibar”.

Amesema Bi Zainab Abdallah

Maadhimisho ya Siku hii ya Wanawake Duniani, Mwaka huu yamepambwa na kauli mbiu isemayo WANAWAKE KATIKA UONGOZI: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa.