Pangani FM

Wanawake 346 wafanyiwa vipimo vya Saratani ya Mlango wa Kizazi Pangani.

3 February 2021, 1:57 pm

Wanawake 346 Wilayani Pangani Mkoani Tanga wamefanyiwa Vipimo vya na kuchunguzwa Saratani ya Mlango wa kizazi Mwaka 2020.

Akizungumza na Pangani FM Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Wilayani Pangani Bi. Edith Chundu amesema kuwa katika idadi hiyo ya Wanawake waliochunguzwa wapo waliokutwa na dalili za awali na kupatiwa ‘TIBA MGANDO’.

“Mwaka 2020, tulichunguza wanawake 346 kati yao wanawake waliokuja wakiwa hawana Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ni 208 kwa kundi hili tuliowakuta na dalili za awali ni 6”Amesema Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na Mtoto Pangani na kuongeza kuwa “Waliokuja kuchunguza saratani wa mlango wa kizazi wakijua wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ni 138 miongoni mwao tuliowakuta wana dalili za awali za saratani ni 10, lakini hao wote tuliwapa Tiba Mgando hapa hapa na tumewapa maelekezo wajitunze vipi”.

Amesema Bi Edith.

Bi. Chundu amesema Takwimu za Mwaka 2019 zinaonyesha ni Wanawake 556 walichunguzwa Saratani hiyo, hivyo ametoa wito kwa wanawake ambao tayari wameshachunguzwa maradhi hayo kurudi tena kuchunguzwa kwa tarehe walizoelekezwa.

“Tuliowachunguza saratani ya mlango wa kizazi mwaka 2019 walikuwa ni 556 na kati yao waliokuja wakiwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi ni 127, sita tuliwakuta na dalili za awali za saratani hii, na 429 walikuwa hawana maambukizi ya virusi vya ukimwi lakini wanawake wanne tuliwagundua kuwa na dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi”. Na kuongeza kuwa“Kina mama ambao tayari mmechunguzwa ni vyema mkarudi tena kuchunguza zitakapofika zile tarehe mlizo takiwa kurudi tena”.

Hayo yanajiri ikiwa kesho Alhamisi Tarehe 4 February ni Siku ya Saratani Duniani, ambapo kwa Mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nchini Mhe. Dorothy Gwajima kwa sasa Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa Saratani wapatao 50,000 na inakadiriwa hadi ifikapo Mwaka 2030 Kutakuwa na Ongezeko la Asilimia 50% la Wagonjwa Wapwa wa Saratani.

Aidha kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni WHO zinaonyesha kwamba mwaka wa 2018 kesi mpya za Ugonjwa wa Saratani Duniani zilikua ni Milioni 18.1 huku watu Milioni 9.6 wakipoteza maisha.

WHO inasema kwamba asilimia 70 ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo wanatoka nchi masikini. Theluthı moja ya waliofariki na ugonjwa wa saratani sababu ilikuwa ni uzito mkubwa wa mwili, matumizi ya sigara na pombe, na kutofanya mazoezi.