Pambazuko FM Radio

Mwanafunzi Mlimba ajeruhiwa kwa viboko na mwalimu

18 May 2021, 7:04 am

Na:Katalina Liombechi

Picha Kutoka Maktaba ya mmoja wa Wanafunzi aliyewai kujeruhiwa kwa Viboko na Mwalimu

Mdau wa Kituo cha Sheria na haki za Binadamu Wilaya ya Kilombero Bashiri Kwahai amewataka walimu kutojichukulia sheria Mkononi kwa kuwaadhibu wanafunzi pasipo kufuata utaratibu kwani ni kinyume na haki za Binadamu.

Hayo ameyasema alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisco hapa Ifakara kumwona Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mlimba Yusuph Napeche ambaye aliadhibiwa kupitiliza na  Mkuu wa Shule  msaidizi   Dikson Myengi, tukio ambalo mwalimu huyo anadaiwa kulitekeleza Mei 10 Mwaka huu.

Amesema kumekuwa na kawaida ya Walimu kuwaadhibu wanafunzi pasipo kufuata utaratibu bila kujali utu wa mtu hivyo wao kama wadau wa sheria watahakikisha haki inatendeka.

Mdau wa Kituo cha Sheria na haki za Binadamu Wilaya ya Kilombero Bashiri Kwahai

Awali Mwanafunzi Yusuph Napeche ameelezea tukio hilo kuwa aliadhibiwa kutokana na Makosa ya Kumpokea Mwanafunzi mwenzao wa Kidato cha Tatu ndipo waliitwa Ofisi ya Walimu na Kuadhibiwa fimbo nane akiwa na wanafunzi wenzake watatu na baadae kuwaita Ofisi ya Taaluma na kuendelea kuwaadhibu fimbo ambazo hazikuwa na Idadi sehemu za Makalio hali iliyopelekea Mwanafunzi Yusuph Napeche kujihisi  maumivu makali na majeraha katika sehemu hizo.

Amesema hali hiyo ilimfanya ashindwe kukaa darasani na kujifunza ,hivyo akawa anasimama na kupiga magoti akiwa Darasani ambapo Mei 11 alipokuwa anatoka Darasani kwenda Mapumziko alijikuta ameishiwa nguvu kutokana na maumuvu hayo wakati akijaribu kushuka kwenye ngazi, alijikuta anshindwa kufanya hivyo hali iliyompelekea kuangaka.

Mwanafunzi Yusuph Napeche

Baba Mzazi wa Mwanafunzi huyo  Hussain Napeche alifanya Taratibu za kumpeleka Kituo cha Afya Mlimba na Baadaye kupata Rufaa Kuja katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko Ifakara Mei 13 Mwaka huu.

Baba Mzazi wa Mwanafunzi huyo  Hussain Napeche

Kwa Mujibu wa Maelezo ya Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisco Ifakara Nassoro Mafunde amekiri kumpokea Mwanafunzi Yusuph Napeche akiwa na Maumivu Makali na Michubuko maeneo ya Makalioni ndipo wakamfanyia vipimo mbalimbali na kuendelea kumpatia Matibabu na Hatimaye Kumruhusu Mei 15 mwaka huu.

Daktari Nassoro Mafunde

Kwa upande wake Mtuhumiwa ambaye ni Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya sekondari Mlimba Dikson Myengi baada ya kufuatwa na Pambazukofm ili afafanue kuhusu tuhuma zinazomkabili,Hakuwa tayari kuongelea hilo

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya sekondari Mlimba Dikson Myengi

Pambazuko Fm imemtafuta Diwani wa Kata ya Mlimba Walaji Abdalah Noti kuzungumzia Juu ya tukio hilo amekiri kulifahamu na kwamba amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa Wazazi juu ya Mwalimu huyo kuwa na kawaida ya kuwaadhibu wanafunzi Kupita kiasi kwa namna hiyo hivyo yeye kama Diwani kwa Kushirikiana na Uongozi wa Kata hiyo wamechukua hatua ya kumtaka Mwalimu huyo kushughurikia Matibabu ya Mwanafunzi Yusuph Napeche kwa Gharama zake huku taratibu zingine za Kumtaka kujieleza Zikifuata.

Kutokana  na kukithiri kwa Vitendo vya kuwaadhibu wanafunzi kinyume na sheria katika Shule hiyo na mwalimu huyo kulalamikiwa Mara kwa mara Diwani huyo pia ameeleza ni vyema Mamlaka Zinazohusika zikaona namna ya kuiangalia Ajira yake.

       CUE IN……DIWANI WALAJI ABDALAH NOTI

Hata hivyo juhudi za kumtafuta Afisa Elimu wa Kata hiyo Mpota bado zinaendelea baada ya simu yake ya mkononi  kuita bila kupokelewa, ili kujua kama tukio hilo analifahamu na nini kinachoendelea.

Imeandaliwa na KATALINA LIOMBECHI PAMBAZUKO FM IFAKARA