Orkonerei FM

watendaji wa halmashauri ya Arusha wametakiwa kuzingatia lishe bora kwa wananchi.

2 April 2022, 8:53 pm

Na. Nyangusi ole sang’da Arusha.

Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuzingatia mkakati wa Serikali juu ya masuala ya Lishe bora ya wananchi katika maeneo yao, kupitia mkataba wa Lishe waliosaini, lengo likiwa kuondoa hali ya udumavu katika jamii na kuwa na jamii yenye afya bora.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango, wakati akifungua kikao kazi cha mkatati wa Lishe, kilichojumuisha Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, halmashauri ya Arusha, chenye lengo la kufanya tathmini ya hali ya lishe kwa miaka mitano iliyopita na kusaini mkataba wa mkakati wa Lishe kwa miaka mitano ijayo, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.

Mhandisi Ruyango, amewaagiza watendaji hao, kuwa na mkakati shirikishi, utakaowashirikisha wananchi, Wahudumu wa Afya, wahudumu wa Afya ngazi ya jamii pamoja na wadau wa maendeleo, kutoa elimu ya Lishe kwa jamii, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata ufahamu juu ya lishe bora, hususani kwa wajawazito na watoto.

“Ninawagiza watendaji wote, Lishe iwe agenda ya kudumu katika vikao vyenu vyote kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata pamoja na menejimenti kwa kuwashirikisha waheshimiwa Madiwani, lengo likiwa kuondoa udumavu wa mwili na akili kwa wananchi wote maeneo yotu, kupitia tathmini ya miaka mitano iliyopita, tunatakiwa kufanya vizuri zaidi kwa miaka mitano ijayo” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewasisitiza Watendaji hao, kuhakikisha kina mama Wajawazito katika maeneo yao wanapata Lishe bora katika siku 1000 za ujauzito, lishe ambayo tafiti zinaonesha ndio inawezesha mtoto aliye tumboni kujenga afya bora ya ubongo na mwili, afya ambayo ndio inategemewa na jamii na Taifa hapo baadaye na kuwasisitiza kutumia vyakula kutoka makundi matano ya vyakula, vyakua ambavyo vinapatikana katika maeneo yote ya Arumeru.

Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amewataka Maafisa watendaji hao, kuhakikisha wajawazito wote katika maeneo yao wanahudhuria kliniki pindi wanapopata ujauzito, wazazi wote wenye watoto wa umri chini ya miaka mitano kuwapeleka watoto hao kliniki, pamoja na kupiga vita tabia ya kina mama wajawazito kujifungulia nyumbani sambamba na kuweka sheria ndogo za kuwashughulikia wale watakaokiuka.

“Ninawasisitiza Maafisa Watendaji wote wa kata na vijiji kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu, ili kuhakikisha wananchi wenu wanakula vyakula kwa kuzingatia makundi yatakayowapa lishe bora, wananchi wakiwa na afya bora nguvu kazi itaongezeka na wananchi wakiwa na nguvu, wataleta maendeleo katika maeneo yetu” ameweka wazi Mkurugenzi Msumi.

Afisa Mtendaji Kata ya Ilboru, Wema Sikoi, amekiri kupata uelewa mkubwa juu ya masuala ya Lishe, na kuahidi kwenda kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na serikali kulingana na mkataba waliousani, na kuongeza kuwa, wataongeza kasi ya kuhakikisha wajawazito wanahudhuria kiliniki na wenza wao, pamoja na kuwapatia lishe bora katika siku 1000 za ujauzito, siku ambazo zinaonekana kuwa ni msingi wa afya ya binadamu yoyote.

Hata hivyo Afisa Lishe, Halmasahuri ya Arusha, Doto Milembe, ameyataja makundi ya vyakula yanayopaswa kuliwa ili mtu kuwa na lishe bora ni vyakula vya nafaka na mizizi, vyakula vya nyama na mikunde, mbogamboga na matunda pamoja na sukari na asali na kubainisha kuwa vyakula vyote hivyo vinapatika katika maeneo mengi ya halmashauri ya Arusha.

Awali serikali imeandaa mpango wa Lishe wa miaka mitano 2022 -2027, unaotaka kila mwananchi kuwa kupata lishe bora kwa kula mlo wenye makundi matano ya vyakula kuanzia siku 1000 za mama mjazito, mtoto anapozaliwa mpaka miaka mitano na jamii nzima, mkakati unaoelekeza kuwasainisha mikataba Maafisa Watendaji wa Kata ili kusimamia mkakati huo wa Lishe.