Orkonerei FM

WAZAZI WAMENUNUA GARI YA KUWAHUDUMIA WAALIMU SHULE YA SECONDARY MWANDET ARUSHA

25 March 2022, 8:18 pm

Gari lililonunuliwa na wazazi wa shule ya ya sekondari mwandet iliyoko arusha.

Na. Nyangusi ole sang’da Arusha.

Wazazi wenye watoto wanaosoma shule ya Sekondari Mwandet, halmashauri ya Arusha, wamekabidhi gari kwa shule hiyo, gari aina ya Coaster yenye namba za usajili T 169 DQX pamoja na kadi ya gari hilo, gari ambalo wamepanga litumiwe na walimu wa shule hiyo, kwenda na kurudi shuleni, makabidhiano yaliyofanyika shuleni hapo wakati wa mahafali ya 5 ya kidato cha sita 2022.

Wakizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, wazazi hao wamesema kuwa, wamesukumwa na changamoto kubwa ya usafiri, iliyokuwa inawakabili walimu wa shule hiyo ya namna ya kufika shuleni kila siku, na kuamua kichangishana fedha za kununua gari, litakalowawezesha walimu kufika shuleni kwa urahisi na kwa wakati.Mwenyekiti wa Kamati ya manunuzi ya gari hilo, Heveanlight Mushi, amesema kuwa, umoja wa wazazi wenye watoto wanaosoma shule ya sekondari Mwandet, wamewiwa kuchangishana fedha za kununua gari, kwa ajili ya walimu wanaowafundisha watoto wao, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na walimu shuleni hapo, ya kuwafundisha wanafunzi huku wakiishi umbali mrefu kutoka shuleni hapo.

Mwenyekiti huyo, ameongeza kuwa, walimu wa shule ya sekondari Mwandet, wanajuhudi kubwa katika kuwafundisha watoto, na matokeo ya juhudi hizo yanaonekana wazi, jambo ambalo limetugusa wazazi wote, na kufanya maamuzi ya kuwanunulia gari, ili kuwarahisishia usafiri wa kufika na kuondoka shuleni kwa wakati.

“Shule ya Mwandeti ni kubwa, ina walimu wengi, haina nyumba za kutosha kuishi walimu wote hapo shuleni, lakini pia eneo hili halina nyumba za kupangisha, hivyo asilimia kubwa ya walimu hulazimika kuishi Ngaramtoni, huku kukiwa hakuna usafiri wa kuaminika kufika shuleni, walimu wanateseka sana, wazazi tumeamua kuwaondolea adha hiyo wakati wakiwahudumia watoto wetu” amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Aidha amefafanua kuwa ununuzi wa gari hilo, umegharimu kiasi cha shilingi milioni 48, fedha zilizopatikana kwa kila wazazi kuchanga kiasi cha shilingi elfu thelathini, jambo ambalo limefanyika kwa muda wa miezi miwili, mara baada ya makubaliano ya wazazi wote.

Akizungumza wakati wa kupokea gari hilo mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, licha ya kuwashukuru wazazi hao kwa, kuwanunulia walimu gari, amewapongeza wazazi hao, kwa moyo wa imani walionao wa kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walimu kwa watoto wao, jambo ambalo wazazi wengi hawatambui wala kuthamini kazi hiyo kubwa inayofanywa na walimu.

Mkurugenzi Msumi, amefafanua kuwa, kutokana na Jiografia ya halmashauri ya Arusha, walimu wa shule nyingi za pembezoni wanakabiliwa na changamoto ya nyumba za kuishi pamoja na usafiri wa kufika shuleni, licha ya kuwa walimu hao, hujitoa kwa hali na mali, kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kufundisha wanafunzi kwa kuweka uzalendo mbele, hivyo wa wazazi hao wamefanya jambo kubwa sana kwa maendelo ya shule ya Mwandet na halmashauri kwa ujumla.

Aidha amewataka, wazazi wengine kuigana mfano huo uliofanywa na wazazi wa Mwandet sambamba na kuwataka wadau wa elimu, kujitokeza kuisaidi serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, hususani katika ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na usafiri.

“Licha ya kuwa serikali imejikita katika kuboresha miundombinu ya shule pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu lakini bado kuna changamoto kubwa ya upungufu wa nyumba za walimu, ukilinganisha na idadi kubwa ya walimu waliopo, hivyo niwakaribishe wadau kuchangia ujenzi wa” amesisitiza Mkurugenzi Msumi

Hata hivyo mkuu wa shule sekondari Mwandet, mwalimu John Masawe, amewasukuru wazazi kwa kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wallimu wa shule hiyo kwa kuwanunulia gari, litakalo rahisisha ussafiri kwa walimu na kuahidi kuendelea kusimamia walimu hao, kuchapa kazi na kupataa matokeo maazuri kwa wanafunzi ili waweze kutimiza ndoto zao.

Shule ya sekondari Mwandet ni miongoni mwa shule za kata, inayoendelea kukua kwa kasi, na kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa, huku ikiwa ni miongozi wa shule 10 bora kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo kwa matokeo ya kidato cha sita.