Nuru FM

Polisi Iringa yawadaka watuhumiwa ubakaji mwanachuo

6 June 2023, 9:32 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP ALLAN BUKUMBI akizungumza na Wanahabari. Picha na Mpiga Picha wetu.

Na Frank Leonard

Jeshi la polisi mkoa wa Iringa limewakamata watuhumiwa watano wa unyang’anyi kwa tumia silaha ambao kati yao wawili wametambuliwa kuhusika katika tukio la ubakaji alilofanyiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (jina linahifadhiwa) wakati wakifanya uharifu chuoni hapo.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi amesema watuhumiwa hao walikamatwa hivi karibuni wakiwa na mapanga matatu, praiz mbili na bajaji namba MC 206 DFF waliyokuwa wakiitumia kufanya uhalifu katika chuo hicho, Semtema, Mkwawa na Mtwivila mjini Iringa.

Amesema katika tukio lililohusisha mwanafunzi huyo kubakwa, watuhumiwa hao walivunja na kuiba vitu mbalimbali kwa baadhi wanafunzi wa chuoni hapo zikiwemo laptop mbili, monita moja na spika zake mbili, simu tatu aina ya TECNO, Guava na iphone pamoja na TV moja aina ya Star X na vocha za TTCL nane.

Kamanda Bukumbi amesema majina ya watuhumiwa wa tukio hilo yamehifadhiwa kwa kuwa bado msako wa kuwanasa watuhumiwa wengine unaendelea kabla hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika tukio lingine ACP Bukumbi amesema jeshi la polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama linaendelea kufanya doria na misako mbalimbali ili kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu.

Katika oparesheni iliyofanyika Juni 4, mwaka huu jeshi hilo kwa kushirikiana na askari wa uhifadhi wamefanikiwa kumkamata David Mapunda (42) mkazi wa Mafinga akiwa na meno mawili ya tembo na kipande kimoja yakiwa katika begi lake dogo.

Katika muendelezo wa msako huo, amesema silaha tatu aina ya gobore zilizotengenezwa kienyeji zimepatikana katika kijiji cha Idodi wilayani Iringa zikiwa zimesalimishwa kwa hiari kutokana na elimu ya kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria inayotolewa na maafisa wa polisi

Katika kata ya Mivinjeni mjini Iringa, amesema jeshi hilo limemkamata Omari Ibrahim (35) akiwa na TV aina ya Hisense inchi 55, RmStar X inchi 32, Kodtec inchi 32, Sumsung inchi 43, CPU aina ya Hp, monita aina ya Dell pamoja na ving’amuzi viwili vya Star Times na Dstv vikidhaniwa kuwa ni mali za wizi.

Alisema watuhumiwa wa matukio hayo watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa pindi uchunguzi utakapokamilika.