Nuru FM

Madiwani Iringa wazuiwa kuingia kikao cha baraza la madiwani

26 May 2023, 9:52 am

Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa Ibrahimu Ngwada akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani. Picha Na Mwandishi wetu

Na Frank Leonard

Madiwani watano na watendaji zaidi ya 10 wamezuiwa kwa zaidi ya saa mbili kuingia katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Iringa kama adhabu baada ya kuchelewa kwenye kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kuanza saa 2:00 asubuhi.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amesema uamuzi wa kuwazuia viongozi hao ni utekelezaji wa maazimio ya pamoja yanayotaka wahusika wote wa vikao vya baraza hilo kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza.

“Kwahiyo hili ni suala la kinidhamu na maadili tu, na tunalishughulikia kimaadili vile vile. Kwasasa hekima yetu imetutaka kuwazuia kushiriki kikao chetu kwa muda wote huo. Ombi langu, tunapokubaliana jambo basi tujitahidi kulitekeleza na kama kuna dharura toeni taarifa lakini sio mje kwenye vikao kwa muda mnaotaka,” alisema Ngwada.

Diwani wa Viti Maalum, Hellen Machibya ambaye ni mmoja wa waliokumbwa na zuio hilo aliomba msamaha kwa niaba ya wenzake na kuahidi kutorudia tena.

Kuzuiwa kwa madiwani na watendaji hao kumewafanya wakose taarifa mbalimbali zilizojadiliwa katika kikao hicho ikiwemo ya fedha na uongozi, ukimwi, uchumi,  afya, elimu na mipango miji na mazingira.

Madiwani wakifuatilia Hoja katika baraza la Madiwani. Picha na Mwandishi wetu

Wakati huo huo mstahiki Meya ameiagiza Menejimenti ya Halmashauri hiyo kuyafanyia matengenezo magari yake yote ambayo yamepaki kwa muda mrefu ili yarudi barabarani na kusaidia kutoa huduma kwa wananchi.

“Matengenezo hayo ni pamoja na ya mitambo yetu tuliyonayo kwa ajili ya matengenezo ya barabara na shughuli za usafi,” alisema Ngwada.

Kuhusu usafi na mazingira Ngwada alizitaka taasisi na watu binafsi kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi wakati wote.

Pamoja na mchango mkubwa wa madiwani kuhusu hali ya barabara katika kata zao, Meya alisema halmashauri hiyo imetenga Sh milioni 10 za mafuta yatakayotumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizoharibiwa wakati wa mvua katika kila kata.