Nuru FM

Baraza la madiwani Iringa lawaonya machinga wanaorejea maeneo yasiyo rasmi

26 May 2023, 9:58 am

Meya Manispaa ya Iringa akitoa agizo. Picha na mwandishi wetu

Na Frank Leonard

Halmashauri ya manispaa ya Iringa imesema hakuna namna wafanyabiashara ndogo (Wamachinga) walioondolewa katika maeneo yasiyo rasmi mjini Iringa wataachwa warudi katika maeneo hayo.

Onyo hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada leo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Verronica Kessy kutoa taarifa inayoonesha baadhi ya wamachinga wameanza kurejea katika maeneo yasiyo rasmi hasa nyakati za jioni.

“Tuna masoko manne kwa ajili ya machinga likiwemo soko la pembezoni mwa makaburi ya Mlandege lililojengwa kwa msaada wa fedha zilizotolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas,” alisema katika kikao cha Baraza la Madiwani .

Wakati madiwani wa baraza hilo wakimpongeza Asas kwa msaada huo waliosema hawatakubali utelekezwe, Ngwada alitaja masoko mengine yaliyojengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao kuwa ni pamoja na magari mabovu, lavela, Isakalilo na ndani ya masoko yote mjini Iringa.

Alisema katika masoko hayo kumewekwa miundombinu yote vikiwemo vyoo vya kisasa pamoja na huduma ya maji na umeme.

“Kwa muktadha huo hakuna namna yoyote ile machinga hao wataachwa warudi katika maeneo yasio rasmi kwasabau zile changamoto walizokuwa wakizilalamikia katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao zimeshughulikiwa.” Alisema Ngwada.

Aidha meya huyo alisema wanayafanyia kazi maombi ya wafanyabiashara hao yanayotaka mnada kuwepo na mnada mmoja tu siku ya jumapili mjini Iringa na ufanyikie katika soko la Mlandege.

“Tumepokea maombi hayo na tunayafanyia kazi. Tunaamini ukianza mnada huo utachochea biashara katika soko Mlandege,” alisema Ngwada.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisema suala la kuwahamishia machinga katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili yao sio suala la kisiasa, ni maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Aliwatahadharisha madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kuyasimamia maelekezo hayo ya Rais vinginevyo akasema wafanyabiashara hao watawapanda vichwani na kurejea katika maeneo yasio rasmi.

“Wameanza kurejea kidogokidogo eneo la mashine tatu; jioni wanakwenda pale na kupanga bidhaa zao, mnawatazama tu. Mkiwaacha kuna siku mtawakuta wote wamerudi pale.” Alisema na kuitaka halmashauri hiyo isisubiri hadi kamati ya ulinzi na usalama ikaingilia kati suala hilo.

Wakati huo huo, DC Kessy ameitaka halmashauri hiyo na mamlaka zinazohusika kusimamia ipasavyo mgawanyo wa njia kwa vyombo vya kusafirisha abiria vinavyotoa huduma katika mji huo.

“Bado bajaji wanaingilia sana njia za daladala. Manung’uniko ya wamiliki wa daladala ni makubwa sana na yanaweza kuathiri utoaji wa huduma hasa kwa abiria wasio na uwezo wa kupanda bajaji,” alisema DC Kessy.