Nuru FM

SYDP laanza kufanya usajili wa washiriki wa mbio za Great Ruaha Marathon 2023

24 May 2023, 2:08 pm

Baadhi ya washiriki wa Great Ruaha Marathon mwaka uliopita. Picha na Mwandishi wetu.

Na Hafidh Ally

Shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) linaloratibu mbio zilizopewa jina la Great Ruaha Marathon 2023 zitakazofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa, tarehe 8 Julai mwaka huu limeanza kufanya zoezi la usajili wa washiriki.

Mbio za Great Ruaha Utalii Marathon zinatarajia kufanyika Julai 8, 2023 kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 500 wakiwemo watalii kutoka nje ya nchi.

Mratibu wa SYDP ambalo ni shirika linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha na ujasiriamali kwa vijana, hifadhi na utunzaji wa mazingira, Hamim Kilahama amesema kuwa mbio zoezi linaloendelea kwa sasa ni kufanya usajili kwa wakimbiaji ambalo linafanyika kwa njia ya mtandao kupitia wavuti yao ya www.greatruahamarathon.co.tz na utakuta kipengele cha kujisajili.

Sauti ya Hamimu akitolea ufafanuzi namna ya kujisajili kushiriki Mbio hizo

Amesema kuwa katika kipengele hicho kitakupa hitaji la aina yam bio ambazo unataka kushiriki kisha utatakiwa kulipa kupitia lipa namba ambayo imewekwa katika wavuti hiyo.

Mratibu wa Great Ruaha Marathon Hamim Kilahama akizungumzia kuhusu Mbio hizo. Picha na Hafidh Ally

“Washiriki watatakiwa kulipa shilingi elfu 45 ili upate nafasi ya kushiriki na hii inawahusisha Raia wa Tanzania huku raia wakigeni wakitakiwa kulipa dola 70, na fedha hizo zitatumika kuhakikisha washiriki hao wanapata huduma za maji, t-shirt ya ushiriki, Verst, medali, huduma za maji katika vituo ambavyo mbio zinapita pamoja na huduma ya chai kwa washiriki wote” alisema Kilahama.

Hamim amebainisha kuwa katika siku zijazo watatangaza vituo ambavyo vitakuwa maalumu Mkoani hapa kwa ajili ya kuwaandikisha washiriki wengine ambao watashindwa kujisajili kwa njia ya mtandao ili kuwafikia wananchi wengi ambao wameonesha nia ya kushiriki katika mbio hizo.

Alisema SYDP inaanda mbio hizi huku ikitarajia kupata ushirikiano kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kupitia hifadhi hiyo ya Ruaha na wadau wengine zikiwemo hotel mbalimbali zilizopo ndani na nje ya hifadhi.

Akizungumzia lengo la kufanya mashindano hayo katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Hamimu alisema kuwa “Tunafanya mbio hizi kwasababu tunataka kukuza utalii katika hifadhi hii ambayo sisi ni wadau wake wakubwa, na tunashirikiana na mamlaka husika ambazo zinaotoa huduma za kitalii kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.”

Mbio hizo za kilometa 5, 10 na 21, na km 42 zitakwenda sambamba na matembezi ya kawaida hifadhini humo.