Nuru FM

Great Ruaha Utalii Marathon kufanyika Ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha Julai 8 2023

19 March 2023, 7:19 pm

Mratibu wa Shirika la SYDP linaloandaa mbio za Ruaha Grat utalii Marathon Hamim Kilahama akizungumzia mbio hizo. Picha na Hafidh Ally

Mbio za Great Ruaha Utalii Marathon zinatarajia kufanyika Julai 8, 2023 kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 600 wakiwemo watalii kutoka nje ya nchi.

Na Hafidh Ally

SHIRIKA la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) linatarajia kuratibu shindano la mbio za marathon zilizopewa jina la Great Ruaha Utalii Marathon  zitakazofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Mkoani Iringa Iringa, tarehe 8 Julai mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa SYDP ambalo ni shirika linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha na ujasiriamali kwa vijana, hifadhi na utunzaji wa mazingira, Hamim Kilahama amesema kuwa Mbio hizo zitashirikisha wakimbiaji zaidi ya 600 wakiwemo watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi katika mataifa mengine.

 “Tumeaandaa Mbio hizi katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha  tukilenga kuhamasisha utalii katika hifadhi hiyo na kutunza mazingira yanayotegemewa na hifadhi vikiwemo vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu, sambamba na kutangaza fursa za uwekezaji na zilizowekezwa ndani na nje ya hifadhi ” alisema Hamimu.

Sauti ya Hamim Kilahama akizungumzia kuhusu Mbio hizo

Aidha Hamim amesema kuwa tayari Mabata Makali Lodge and Campsite wameshaonesha nia ya kudhamini huku akawakaribisha wadau wengine wa utalii kuwadhamini mbio hizo za kilometa 5, 10 na 21 ambazo zitakwenda sambamba na matembezi ya kawaida hifadhini humo.

Alisema SYDP inaanda mbio hizi huku ikitarajia kupata ushirikiano kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kupitia hifadhi hiyo ya Ruaha na wadau wengine zikiwemo hotel mbalimbali zilizopo ndani na nje ya hifadhi.

Alisema kabla ya kufanyika kwa mbio hizo SYDP itaratibu pia ligi ya mpira wa miguu itakayoshiriki timu za vijiji vyote vya tarafa ya Idodi vinavyozunguka hifadhi hiyo ili itumike kufikisha elimu ya malengo ya mbio hizo.

Meneja wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Nyemo Lekuona akizungumzia jinsi walivyojiandaa kupokea wageni watakaoshiriki Mbio hizo. Picha na Hafidh Ally

Kwa upande wake Meneja wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Nyemo Lekuona alisema; “Tutadhamini mbio hizi kwasababu tunauona mchango wake katika kukuza utalii katika hifadhi hii ambayo sisi ni wadau wake wakubwa tunaotoa huduma za kitalii kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.”

Mbali na kudhamini alisema wanaendelea kujipanga kikamilifu ili kuhakikisha wageni watakaokuja kushiriki mbio hizo wanapata huduma zitakazowawezesha kurudi mara kwa mara katika hifadhi hiyo ili kujionea vivutio vyake.

Sauti ya Meneja wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Nyemo Lekuona akizungumzia huduma wanazotoa katika eneo lao
Mkurugenzi wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Eward Athanas akiwakaribisha wadau wengine kudhamini mbio hizo. Picha na Hafidh Ally

Mkurugenzi wa Mabata Makali Lodge and Campsite, Eward Athanas alisema; “Hii ni mara ya pili kwa hoteli yetu kudhamini mbio hizo zilizoanza mwaka jana. Tunaomba makampuni na taasisi zingine zituunge mkono kwani mbio hizo zina faida kubwa katika kuindeleza sekta yetu ya utalii.”

Alisema kwa mara ya kwanza mbio hizo za Great Ruaha Utalii Marathon zilifanyika mwaka jana kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya 100 katika eneo la hotel yake hiyo iliyopo nje ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Mwaka huu mbio hizi zinafanyika ndani ya hifadhi na idadi ya wakimbiaji inatarajia kuongezeka na kuzifanya kuwa kubwa zaidi hivyo ni muhimu wadau wengine wakajitokeza kuuinga mkono SYDP ili izifanikishe,” alisema.

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni ya pili kwa ukubwa nchini baada ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ni maarufu kwa idadi kubwa ya Tembo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 10,000 sambamba na kuwa na wanyama aina ya kudu wakubwa na wadogo, pofu, simba, chui, nyati, pundamilia, mbweha, fisi, mbwa mwitu, mamba, viboko, twiga, swala pala, ndege zaidi ya 500 na mimea karibu yote inayopatikana kusini na mashariki mwa Afrika.