Nuru FM

Nyumba ya walemavu Lulanzi iliyochangiwa Mil. 5 na Waziri Mkuu yakamilika

7 March 2023, 12:38 pm

Balozi wa Utalii Tanzania Isabella Mwampamba Mwenye Kilemba Chekundu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nyumba ya walemavu Lulanzi. Picha na Hafidh Ally

Ujenzi wa Nyumba ya walemavu wanaoishi Kijiji cha Lulanzi umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 26 huku kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 5 zikitolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Hafidh Ally

Hatimaye Nyumba kisasa ya walemavu watatu wa familia moja wa kijiji cha lulanzi Kilichopo Kata ya Mtitu Wilaya ya Kilolo iliyokuwa inajengwa kutokana na Michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo chini ya Taasisi ya Isabella Foundation imekamilika.

Akizungumza wakati wa kukabidhi nyumba hiyo kwa familia hiyo Balozi wa Utalii Nchini Isabella Mwampamba ambaye ni Mkurugenzi wa Isabella Foundation amesema kuwa ujenzi huo umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 26 huku kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 5 zilitolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa.

Balozi wa Utalii Nchini Isabela mwampamba akizungumzia ujenzi wa nyumba hiyo

“Kipekee nimshukuru sana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutuunga Mkono katika mradi huu wa ujenzi wa nyumba ya walemavu hawa watatu ambao kwa kweli walikuwa wakiishi katika mzingira magumu, ” alisema Isabella

“Kipekee nimshukuru sana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutuunga Mkono katika mradi huu wa ujenzi wa nyumba ya walemavu hawa watatu ambao kwa kweli walikuwa wakiishi katika mzingira magumu, ” alisema Isabella

Aidha Balozi Isabella amebainisha kuwa licha ya Nyumba hiyo kukamilika na kuikabidhi kwa familia hiyo bado kuna madeni ambayo bado wanadaiwa kiasi cha shilingi Milioni 10 kutoka kwa Mafundi waliopewa tenda ya ujenzi ambao ni Chuo Cha RDO Kilolo, Kampuni ya usambazaji wa vifaa vya ujenzi General Supplies, huku akiwaomba wadau wa maendeleo kushiriki katika kusaidia kulipa deni hilo na kununua mahitaji mengine,

Akizungumza huku akibugujikwa na machozi ya Furaha wakati wa kukabidhiwa nyumba hiyo, Mama Mzazi wa walemavu hao watatu Bi. Anjelista Kihanza amesema kuwa anashukuru kwa kujengewa nyumba hiyo kwani hapo awali walikuwa wakiishi katika nyumba ambayo inavuja huku akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Balozi Isabella na ofisi ya Wilaya ya Kilolo kwa kushiriki kufanikisha ujenzi huo.

Mama Mzazi wa walemavu hao watatu Bi. Anjelista Kihanza akitoa shukrani baada ya kukabidhiwa nyumba

“Kwa kweli kama siyo Balozi Isabella kuja na kuamua kuwajengea nyumba hiyo, watoto hawa wangefariki dunia kwani wazo lake limesaidia kumleta Waziri Majaliwa kutoa fedha ambazo zimesaidia ujenzi wa nyumba hii, Mungu awabariki kwa kila jambo” alisema Mama Mzazi wa Walemavu hao Bi. Anjelista.

Awali walemavu hao wameshukuru kwa kujengewa nyumba hiyo ya kisasa huku wakifurahia zaidi kuwepo kwa choo na bafu ndani hali ambayo inawasaidia kwa sasa kutopata shida pindi wanapotaka kwenda maliwatoni.

Kwa upande wake Rahman Mkakatu ambaye ni Diwani wa Kata ya Mtitu na Luca Idd Kihongosi Ni mwenyekiti wa Kijiji Cha Lulanzi amewashukuru wananchi wa Kijiji cha lulanzi na wadau wa maendeleo kwa ujumla kwa kuamua kutatua shida walizokuwa nazo hasa changamoto ya ubovu wa Nyumba ambayo ndio ilikuwa kubwa, ukosefu wa maji na umeme.

Nyumba hiyo ya kisasa yenye vyumba Viwili vyenye choo na bafu ndani na sebule ilianza rasmi ujenzi wake mwezi wa Tano mwaka 2022, imezinduliwa Rasmi huku viongozi wa Dini wakifanya ibada ya kubariki nyumba ili Familia hiyo iweze kuishi katika mazingira bora.