Nuru FM

Mangungu ashinda uchaguzi wa Simba Sc

30 January 2023, 6:49 am

Mwanachama wa Simba SC Murtaza Mangungu amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Kupitia Mkutano Mkuu wa Uchaguzi 2023.

Mkutano huo ulianza jana Jumapili (Januari 29) na kumalizika leo Jumatatu (Januari 30) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ‘JNICC’ jijini Dar es salaam.

Matokeo ya Uchaguzi huu yamechelewa kutangazwa kutokana na zoezi la kuhesabu kura kuchukua muda mrefu, kutokana na idadi kubwa ya Wanachama waliojitokeza kupiga kura.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC Boniface Lihamwike alimtangaza Mangungu kushinda uchaguzi huo, akipata kura 1311 dhidi ya mpinzani wake Adv. Moses Kaluwa aliyepata kura 1045.

Kwa mantiki hiyo Mangungu anaendelea kuwa Mwenyekiti wa Simba SC kwa kipindi cha miaka minne, baada ya kuiongoza Klabu hiyo kwa miaka miwili tangu 2021.

Mwenyekiti wa Simba SC Murtaza Mangungu akiwa na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC baada ya kutangazwa na Kamati ya Uchaguzi

Kwa upande wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walioshinda ni Dr Seif Ramadhan Muba (1636), Asha Baraka (1564), CPA Issa Masoud Iddi (1285), Rodney Chiduo (1267) na Seleman Harubu (1250).

Jumla ya Wanachama Simba SC waliopiga Kura ni 2363 Kura halali, lakini Kura halali zilikuwa 2356.