Nuru FM

MNEC Salim Asas ampongeza Rais Samia kwa kutunukiwa shahada ya heshima

1 December 2022, 11:16 am

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kutunukiwa shahada ya juu ya  udaktari  wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutokana na kufanya mabadiliko ya kimaendeleo tangu alipoingia madarakani Machi 2021.

Rais Samia ametunukiwa udaktari huo  jana Novemba 30, 2022 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Jakaya Kikwete kwenye mahafali ya 52 ya Chuo hicho  yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Milmani City uliopo  jijini Dar es Salaam.

MNEC ASAS amesema heshima hiyo aliyopewa Rais Dkt. Samia Suluhu imeonesha imani ya wananchi wa Tanzania kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kuboresha maisha katika sekta mbalimbali.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas

Akizungumza mara baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia ameushukuru uongozi wa UDSM kwa kutambua na kuona mchango wake anaoufanya ndani ya nchi ya Tanzania huku akikiri kujaribu kuitafuta shahada hiyo lakini muda haukumpa nafasi.

“Suala la kupewa tuzo hii nimelipokea kwa unyenyekevu mkubwa, nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi,” amesema Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza baada ya kutunukiwa shahada ya heshima

Miezi 11 iliyopita kiongozi hiyo mkuu wa nchi alisema alitamani kujiendeleza kimasomo lakini majukumu yalimzuia lakini tukio hilo limekamilisha ndoto yake ya kuwa daktari wa heshima

Maazimio ya senenti ya Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kikao chake cha 875 yalimpendekeza Rais Samia kutunukiwa shahada hiyo kutokana na mabadiliko makubwa yaliyoletwa na uongozi wake.