Nuru FM

Asilimia 60 Ya Misitu Ya Vijiji Morogoro Yavamiwa, Mashirika Ya Tfcg Na Mjumita Yapongezwa

22 November 2022, 5:28 am

Wakazi wa Mkoa wa Morogoro wametakiwa kuepukana na vitendo vya uharibifu wa Mazingira katika Mkoa huo badala yake washiriki kikamilifu katika utunzaji kwakuwa mkoa huo umekuwa na mchango Mkubwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es salaam na Pwani.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro Joseph Joachim Chuwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa takriban asilimia 60 ya misitu ya vijiji imevamiwa kwa sababu ya Kilimo kisichoendelevu,ukataji wa miti hovyo na utengeneza wa mkaa.

Chuwa amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) kwa kutoa elimu ya usimamizi shirikishi wa Misitu na Uvunaji endelevu wa misitu katika vijiji 35 pamoja na uanzishwaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Halmashauri ya Mvomero,Morogoro na Kilosa  kupitia Mradi wa Usimamizi shirikishi wa misitu ya Jamii (USMJ) chini ya Mradi wa kuleta mageuzi katika ya mkaa Tanzania (TTCS) .

Amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika Mradi huo hasa baada ya jamii kutambua namna inavyoweza kunufaika na misitu inayowazunguka kwa kuivuna kwa uendelevu na hivyo kupata mwamko ambao umesaidia kuimarisha utunzaji wa misitu na kupelekea nchi zingine kama vile Zambia  kuja Tanzania tena Morogoro kujifunza mbinu ya utunzanji wa misitu ya asili katika vijiji.

Chuwa amesema kuwa kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za serikali  pamoja na wadau wa aendeleo wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya Uhifadhi wa mazingira na misitu Ili kuhakikisha inahifadhiwa ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.

“Namshukuru sana Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhifadhi Mazingira akishiriki kwenye mikutano mbalimbali ya Kimataifa inayolenga kuhifadhi Mazingira nchini.

Chuwa amewakumbusha watanzania kufahamu kuwa Uhifadhi wa mazingira sio jambo la mtu Mmoja au viongozi pekee bali ni la watu wote walioumbwa katika Dunia hivyo  ni jukumu la kila mtu kuepukanana na madhara yanayotokana na uharibifu wa Mazingira.

Amesema ili kunusuru Hali ya uharibifu wa Mazingira na misitu wadau kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama vile hawa TFCG na MJUMITA wanafanya kazi kubwa ya  kuiunga Mkono serikali Ili kuhakikisha  misitu hiyo inalindwa na kuhifadhiwa.

“Katika hizi Wilaya ya tatu ya Kilosa,Mvomero na Morogoro Pamoja na vijiji 35 ambavyo vimeingia katika mpango wa matumizi endelevu ya misitu hiyo tumeona mafanikio makubwa kwani wananchi na vijiji wamenufaika nayo sana,”ameeleza Bw. Chuwa.

Kuhusu Mapato waliyopata mwaka 2021/2022 ambayo yameingia kwenye serikali kuu, Halmashauri na Wilaya ni Takriban zaidi ya  Bill. 2 ambapo vijiji 35 kwa kupitia uvunaji wa misitu endelevu vina zaidi ya Bill 1.6 na kama tutafanikiwa kuviingiza vijiji vyote 129 katika mpango huu wa kuvuna Kwa njia endelevu itasaidia kuwa na Maendeleo makubwa katika vijiji hivyo

Ameeleza kuwa kupitia miradi hiyo pia serikali za vijiji vimenufaika na mpango huo kwa kujenga miundombinu ya afya shule ofisi za serikali na mengine mengi kwani lengo lao ni kuokoa misitu na hivyo mkaa endelevu unavunwa katika hali ambayo inaokoa misitu kwa kiwango kikubwa wakati huohuo wanafanya aendeleo katika vijiji vyao

Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ)  ulikuwa unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwa ufadhili wa Shirika la  Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).