Nuru FM

Kauli ya Nape malalamiko ya kupunjwa ‘bando’

11 November 2022, 5:24 am

Waziri wa Mawasiliano Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape amesema wizara yake imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuwaita watoa huduma baada ya kutokea sintofahamu ya bei ya vifurushi.

Spika Dk Tulia Ackson amemtaka Waziri huyo kufafanua uwepo wa utata wa bei katika vifurushi akinukuu taarifa ya mteja aliyetaka kununua kiasi cha GB 1 lakini akapata MB 800, ikiwa ni pungufu ya MB 200 ya mahitaji yake ikilinganishwa na bei iliyotangazwa.

Kuhusu hilo, Nape ameliambia Bunge kuwa kila baada ya miezi mitatu, watoa huduma wanakuwa na uwezo wa kubadili gharama ya vifurushi.

Hata hivyo mabadiliko hayo hutakiwa kuonekana katika ‘menyu’ ikionesha kiwango na gharama.

Kilichotokea, kwa mujibu wa Waziri, ni kwamba mtoa huduma hakuhuisha taarifa katika bango [menyu].

Wizara imeiagiza TCRA iwaite watoa huduma juu ya suala hilo, ameongeza Waziri.

Suala la vifurushi limeibuka bungeni, Dodoma leo wakati Mbunge wa Mkalama, Francis Mtinga akichangia hoja katika mapendekezo ya Mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali na mapendekezo ya Mpango Wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24.

Mbunge huyo amehoji ikiwa sheria inaweza kutungwa ya kuwabana watoa huduma ya mawasiliano juu ya ukomo wa muda kwa vifurushi akihusisha na ‘wizi’.

Nape aliomba mwongozo kwa lengo la kutoa ufafanuzi na Spika alipompa fursa hiyo akasema: “Bando ni huduma ya ziada.”

Amesema ipo njia ya bila kununua vifurushi ambavyo havina ukomo wa muda ambavyo vinapatikana kupitia “main tariffs.”

Amesema vifurushi ni suala la kibiashara na si la kisheria huku akisisitiza “nadhani kushutumu ni kuharibu..”